Fahamu kwa nini gavana Gladys Wanga ametangaza Ijumaa Mei 5 siku ya likizo Homabay

Wanga alisema kuwa hakuna afisa wa kaunti yake atakayechukuliwa hatua za kinidhamu kwa kukosa kufika kazini Ijumaa.

Muhtasari

• Wanga alisema wafanyikazi katika sekta muhimu kama hospitali, usalama na wakusanyaji ushuru ni sharti wafike kazini.

Gavana Wanga atangaza likozo Ijumaa Mei 5 Homabay.
Gavana Wanga atangaza likozo Ijumaa Mei 5 Homabay.
Image: Facebook

Kwa hali ya kushangaza, gavana wa kaunti ya Homabay Gladys Wanga ametangaza siku ya Ijumaa Mei 5 kuwa siku ya mapumziko kwa wafanyikazi wote wa kaunti hiyo ili kupisha nafasi kwa riadha za kilomita 21 ambapo zinalenga kutoa hamasisho la kijamii kwa kulinda mbuga ya wanyama ya Ruma.

Akizungumza siku moja iliyopita katika maandalizi ya marathon hizo, Wanga alisema kuwa Ijumaa Mei 5 hadi Mei 6 ambayo ni JUmamosi zitakuwa siku za mapumziko kuruhusu watu kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo.

Mbio hizo zinanuia kutoa hamasisho la kuwatunza swala ambao wako katika ukingo wa kutokomea kabisa kwa jina Roan.

Takwimu za shirika la wanyamapori zinakisia kwamba swala hao adimu wamesalia 25 tu nchini Kenya na wote wako katika mbuga ya Ruma inayopatikana katika kaunti hiyo ya Homabay.

“Mei 5 itakuwa siku ya mapumziko kwa kaunti kuruhusu watu kushiriki katika marathoni, isipokuwa tu kwa wafanyikazi kwenye sekta muhimu. Wahudumu wa hospitalini hamwezi toka na muache hospitali bila mtu, pia watu wa ulinzi hamwezi shiriki katika riadha hizo. Wakusanyaji ushuru lazima wachukue ushuru..” gavana Wanga alisema.

Mkuu huyo wa kaunti alibaini wageni wanaokwenda kwenye mbuga hiyo ni watu kutoka sehemu zingine.

“Tuna watu ambao wamezaliwa hapa Homabay lakini hawajawahi kwenda Ruma. Hii ni fursa ya kwenda huko na kuona mbuga hiyo,” Bi Wanga alisema.

Aliwaambia wafanyikazi wake kwamba hakuna hatua zitachukuliwa dhidi yao ikiwa hawataripoti ofisini Ijumaa.

Pia aliagiza wakuu wa idara kupanga jinsi wafanyikazi wanaweza kuhudhuria mbio za marathon.

Sheria ya Kenya inaelekeza kwamba ni waziri pekee anayesimamia Wizara ya Mambo ya Ndani anaweza kutangaza kihalali sikukuu ya umma.

Lakini pia inafahamika kubwa tangazo la Wanga kwa wafanyikazi wa kaunti halina maana ya kuwa ni sikukuu ya mapumziko bali ni tuhusa kwa wafanyikazi na watu wake kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika hamasisho hilo,