DP Gachagua ajivunia bei ya msokoto wa bangi kupanda kutoka 100 hadi 400

Gachagua alidokeza kuwa mihadarati hiyo imekuwa ghali sana isiweze kununuliwa na watumiaji wengi.

Muhtasari

•Gachagua alibainisha kwamba bei ya bangi katika eneo la Kati imeongezeka sana tangu vita dhidi ya mihadarati kutangazwa, jambo ambalo kulingana naye, ni hatua muhimu sana.

•Naibu rais sasa ametoa wito kwa hatua kama zilizochukuliwa dhidi ya bangi kuchukuliwa dhidi ya pombe.

akitoa hotuba wakati wa kongamano la mashauriano mjini Naivasha mnamo Mei 4, 2023.
Naibu rais Rigathi Gachagua akitoa hotuba wakati wa kongamano la mashauriano mjini Naivasha mnamo Mei 4, 2023.
Image: FB// DP RIGATHI GACHAGUA

Naibu rais Rigathi Gachagua amejivunia maendeleo makubwa katika vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya katika eneo la kati.

Akizungumza wakati wa kongamano la mashauriano ambalo lilifanyika mjini Naivasha siku ya Alhamisi, kiongozi huyo wa pili kwa utawala alibainisha kwamba bei ya bangi katika eneo la Kati imeongezeka sana tangu vita dhidi ya mihadarati kutangazwa, jambo ambalo kulingana naye, ni hatua muhimu sana.

"Nina furaha sana kwamba tangu tuanze zoezi hili katika eneo la kati mwa Kenya, msokoto wa bangi ambao ulikuwa ikiuzwa kwa shilingi mia moja sasa unauzwa 400. Wanapiga hatua. Hayo ni maendeleo mazuri,"  alisema.

Gachagua alidokeza kwamba mihadarati hiyo imekuwa ghali sana isiweze kununuliwa na watumiaji wengi.

“Hilo ni jambo sahihi. Kwa kuwa sababu polisi wanafuatilia bangi sana, wale wanaouza, kwa kuwa hatari iko juu sana wanaongeza pesa, wakiuza 400 waliokuwa wanamudu 100 wanaacha sigara kwa sababu haipatikani," alisema.

Kufuatia hayo, naibu rais sasa ametoa wito kwa hatua kama zilizochukuliwa dhidi ya bangi kuchukuliwa dhidi ya pombe.

Alisikitika  kwamba vijana wengi wanakunywa pombe kwa sababu inapatikana rahisi na kwa bei nafuu madukani.

"Tufanye iwe vigumu kuwa na pombe ya bei nafuu. Waacha vijana hawa waende wakafanye kazi kama wanataka kunywa Tusker, ambayo ni shilingi 200. Aende afanye kazi, alipwe mia nne, akunywe mbili iishe bila chakula," alisema.

Aliongeza, "Hii pombe ya shilingi 30 na shilingi 40 ndiyo shida. Hata kama tunasema  tunahitaji kuunda mambo mbadala kwa wavulana hawa, kama serikali , kama jamii tumeruhusu sumu kwenye maduka kwa bei nafuu."

Naibu rais alilalamika kwamba tembo imewafanya vijana kulegea na kushindwa kufanya kazi za kawaida ili kujisimamia.

Alizungumza Alhamisi wakati wa ufunguzi wa kongamano la siku tatu  la mashauriano ambalo linawaleta pamoja wawakilishi wadi, maseneta, mashirika ya uchunguzi, waendesha mashtaka, watayarishaji wa sheria, NACADA, KEBS, mashirika ya kupambana na bidhaa ghushi na washikadau wengine kutoka kaunti za eneo la kati zikiwemo Kiambu, Nyeri, Murang'a, Nyandarua, Kirinyaga na Nyeri.