Metro Trans wafuata nyayo za Super Metro, wazindua mabasi 5 ya umeme Nairobi

Kampuni hiyo ilitangaza kuwa ni njia moja ya kutoa mchango wa kudhibiti uchafuzi wa hali ya hewa jijini Nairobi.

Muhtasari

• Kama njia moja ya kuwathamini wateja wao, kamouni hiyo ilitangaza safari za bila malipo kutoka jijini kwenda Utawala.

Basi la umeme la Metro Trans.
Basi la umeme la Metro Trans.
Image: Facebook

Kampuni ya mabasi ya Metro Trans imezindua mabasi mapya 5 yanayotumia umeme jijini Nairobi.

Kupitia ukurasa wao wa Facebook, Metro Trans ambao ni washindani wakuu wa Super Metro walipakia picha za mabasi hayo matano na kusema kuwa ni furaha yao kuendeleza kuhimiza matumizi ya magari ambayo hayachafui hali ya hewa.

“Tumefurahi kupokea mabasi 5 mapya kabisa ya BasiGo 100% ya umeme leo jijini Nairobi. Tumejitolea kukuhudumia vyema kwa usafiri salama, nafuu na laini. Mungu akubariki kwa kuendelea kutuunga mkono,” Metro Trans walidokeza kwa fuaha.

Kampuni hiyo ilibaini kuwa ilitoa usafiri wa bure kwenda Utawala ili kuwathamini wateja wake. Mabasi hayo yalizinduliwa kwa ushirikiano na Basi Go, shirika la e-mobility linalolenga kuleta mapinduzi katika sekta ya uchukuzi wa umma kwa kuwapa wamiliki wa mabasi ya usafiri wa umma njia mbadala ya umeme kwa gharama nafuu badala ya dizeli na petroli.

“Kampuni ya uchukuzi ya MetroTrans EA Limited twakaribisha mabasi yanayotumia nguvu za umeme jijini Nairobi. Tutadhibiti uchafuzi wa hewa na mazingira. Asanteni wateja wetu!” walitangaza.

Mabasi ya umeme.
Mabasi ya umeme.
Image: facebook

Jumanne, Februari 14, kamouni pinzani ya Super Metro ilizindua basi lake la kwanza la umeme. Basi hilo lenye uwezo wa kubeba watu 25 litasafiri kati ya Nairobi CBD hadi Kitengela na njia ya CBD hadi Kikuyu.

Mwenyekiti wa Sacco hiyo Nelson Mwangi Nduki alieleza kuwa kuongezwa kwa basi hilo la umeme kwenye meli yake kutawasaidia kutoa huduma kwa wateja.

"Tumenunua basi ili kuwapa wateja wetu uzoefu wa hali ya juu na tunatarajia kusikia maoni chanya kutoka kwa madereva na abiria wetu," alisema.