Biblia ya kale ya Kiebrania yauzwa kwenye mnada kwa dola milioni 38

Codex Sassoon inasadikiwa kuwa iliandikwa miaka 1,100 iliyopita.

Muhtasari

•Biblia ya kale ya Kiebrania imenunuliwa huko New York Marekani kwa dola milioni 38.1, na kuwa hati ya thamani zaidi kuuzwa kwa mnada.

•Zabuni iliyoshinda ilizidi dola milioni 30.8 iliyolipwa na mwanzilishi mwenza wa Microsoft Bill Gates mnamo 1994 kwa Codex Leicester, daftari la kisayansi la Leonardo da Vinci.

Image: BBC

Biblia ya kale ya Kiebrania imenunuliwa huko New York Marekani kwa dola milioni 38.1, na kuwa hati ya thamani zaidi kuuzwa kwa mnada.

Codex Sassoon inasadikiwa kuwa iliandikwa miaka 1,100 iliyopita.

Ni kielelezo cha mapema zaidi cha hati moja iliyo na vitabu vyote 24 vya Biblia ya Kiebrania yenye alama za uakifishaji, vokali na lafudhi.

Mwanasheria wa Marekani na balozi wa zamani Alfred Moses aliinunua kwa ajili ya Jumba la Makumbusho la ANU la Watu wa Kiyahudi huko Tel Aviv, Israel.

"Biblia ya Kiebrania ndiyo yenye ushawishi mkubwa zaidi katika historia na ni msingi wa ustaarabu wa Magharibi," Bw Moses alisema katika taarifa.

Zabuni iliyoshinda ilizidi dola milioni 30.8 iliyolipwa na mwanzilishi mwenza wa Microsoft Bill Gates mnamo 1994 kwa Codex Leicester, daftari la kisayansi la Leonardo da Vinci.

Lakini haikufikia rekodi ya hati ya kihistoria iliyouzwa kwa mnada iliyowekwa na meneja hazini ya wawekezaji Ken Griffin, ambaye alinunua nakala ya kwanza iliyochapishwa ya katiba ya Marekani kwa dola milioni 43.2 miaka miwili iliyopita.

Codex Sassoon imepewa jina la mmiliki wa awali, David Solomon Sassoon, ambaye aliipata mwaka wa 1929 na kuweka mkusanyiko mkubwa zaidi wa kibinafsi wa hati za Kiebrania duniani nyumbani kwake huko London.

Maandishi ya Biblia ya Kiebrania - ambayo vitabu vyake 24 vinajumuisha kile ambacho Wakristo wanakiita Agano la Kale - yaliendelea kubadilika-badilika hadi Enzi za mapema za Kati, wakati wasomi wa Kiyahudi wanaojulikana kama Wamasora walipoanza kuunda maandishi kadhaa ambayo yalisawazishwa.