Harusi ya ajabu!Wanandoa viziwi wafunga pingu za maisha katika harusi ya kipekee

Harusi hiyo ilivutia mamia ya waumini kushuhudia sherehe hiyo ya kipekee.

Muhtasari
  • Makokha ambaye ndiye aliyeongoza harusi hiyo pia alitegemea wakalimani kufikisha ujumbe kwa wanandoa hao.
Pete
Pete
Image: SERENDIPITY DIAMONDS

Kwa kweli hawakukosea waliposema 'disability is not in ability' hayo ni maneno waliyo ya dhibitisha wanandoa wawili kaunti ya Nakuru siku ya Jumapili Mei28/2023 baada ya kufunga pingu za maisha.

Wapenzi hao walipeana viapo vya kimyakimya kwa usaidizi wa wakalimani wa lugha ya ishara katika harusi ya kupendeza kanisani ambayo iliwashangaza wakazi mjini Nakuru.

Jenifer Wanja, 24, alifunga ndoa na Bethwel Kinyua mwenye umri wa miaka 41 katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Francis mjini Nakuru.

Harusi hiyo ilivutia mamia ya waumini kushuhudia sherehe hiyo ya kipekee.

"Yeye ni mtu anayejali, na ananipenda kwa dhati," Wanja alisema kupitia kwa mkalimani.

Kuanzia viapo hadi hotuba, kila kitu kilifanyika kwa lugha ya ishara ili kuhakikisha wanachama wote waliohudhuria wanafuata shughuli zilivyokuwa zikiendelea.

Baada ya kuapisha viapo vya ndoa, nyuso zao ziliangaza kwa furaha kuashiria furaha yao ya ndani na kuridhika kwa ndoto hiyo.

Tangu wakutane mnamo 2022 huko Mukurweini, Kaunti ya Nyeri, kwenye hafla ya kanisa, wapenzi hao hawakuweza kuficha mapenzi yao.

"Nilienda kufanya kazi huko Mukurweini na kukutana na Jenifer, nikazungumza na wazazi wake na kumleta Nakuru hapa," Bethwel alieleza.

Babake alibainisha kuwa Wanja alifurahi sana alipokutana na mpenzi wake.

“Alikuja na kuniambia amepata mapenzi na yuko tayari kwa ndoa. Nilimpa ruhusa na kumtakia heri katika ndoa yake. Nina furaha siku hiyo ilifanikiwa,” babake Wanja alisimulia.

Mamake Jenifer Mercy Wambui, kwa upande mwingine, alifichua kwamba alikuwa akiombea bintiye apate mume ambaye angemwelewa.

"Alipokuwa mchanga, nilikuwa nikimwomba Mungu ambariki kwa mwanamume ambaye pia ni kiziwi ili waelewane kwa urahisi," alifichua Mercy Wambui.

“Nina furaha mwanangu sasa ameolewa. Nawatakia baraka za Mungu katika safari hii ya maisha mapya,” akasema babake bwana harusi Titus Kinyua.

Makokha ambaye ndiye aliyeongoza harusi hiyo pia alitegemea wakalimani kufikisha ujumbe kwa wanandoa hao.