Hata mimi ni mtoto wa Ramogi na sijisifu - Gaucho kwa Gachagua kujiita mtoto wa Mau Mau

Uulichaguliwa kuweka mlima Kenya wakuwe sawa katika mambo ya maziwa, kahawa, majani chai na mambo ya Miraa kule Meru - Gaucho alimwambia Gachagua.

Muhtasari

• Kwa mujibu wa mkosoaji huyo wa serikali, hata yeye ni mtoto wa Ramogi lakini haendi kila mahali akijitapa.

• Gaucho alikamatwa tena siku mbili zilizopita na kufikishwa katika mahakama ya Kiambu ambako alishtakiwa kwa kujaribu kuzua fujo.

Gaucho amzomea vikali naibu wa rais Rigathi Gachagua kujiita mtoto wa Mau Mau.
Gaucho amzomea vikali naibu wa rais Rigathi Gachagua kujiita mtoto wa Mau Mau.
Image: Facebook

Mtetezi mkali wa Azimio ambaye pia ni rais wa bunge la mwananchi Gaucho baada ya kuachiliwa kwa bondi katika mahakama ya Kiambu ametoa tamko kali kwa serikali na safari hii akimlenga naibu rais Rigathi Gachagua.

Gaucho alimwambia Gachagua kwamba alichaguliwa kufanyia wananchi wa Kenya kazi na si kwenda kila mahali akiwatishia wananchi kwa kujitapa kuwa yeye ni mtoto wa Mau Mau.

Kwa mujibu wa mkosoaji huyo wa serikali, hata yeye ni mtoto wa Ramogi lakini haendi kila mahali akijitapa.

“Mimi ninaambia Gachagua, rafiki yangu hukuchaguliwa kutishia watu na Mau Mau. Eti ukienda mahali ni mau mau , ukienda sijui wapi ni mau mau, ulichaguliwa kuweka mlima Kenya wakuwe sawa katika mambo ya maziwa, kahawa, majani chai na mambo ya Miraa kule Meru. Haukuchaguliwa ya kwamba ukiendqa kila mahali wewe ni mtoto wa mau mau, hata mimi ni mtoto wa Ramogi na sijisifu,” Gaucho alizungumza kwa machungu.

Awali, kwa mujibu wa DCI, Gaucho alikuwa amefikishwa katika mahakama ya Kiambu na kusomewa mashtaka ya kujaribu kuzua fujo lakini akakanusha na kuachiliwa kwa dhamana.

“Mapema leo, Calvin Okoth Otieno almaarufu "Gaucho" alifikishwa mbele ya mahakama za Kiambu kwa tuhuma za kuleta fujo kinyume na kifungu cha 95 (1)(b) cha kanuni ya adhabu. Mshukiwa alikana mashtaka na kuachiliwa kwa bondi ya Sh20,000 au dhamana ya pesa taslimu Sh5,000,” DCI waliripoti kupitia mitandao yao ya kijamii.

Gaucho amekuwa akikwaruzana na vyombo vya dola kaitka siku za hivi karibuni katika kile ambacho serikali wanasema mkutano wake wa bunge la wananchi ambako anaikosoa vikali serikali ni wa kuleta fujo.