Reuben Kigame alia kupokea Ksh 1295 kutoka PRISK licha ya kuwa na albamu 30

"Katika maisha yangu yote ya kimuziki, sijawahi pewa hata nusu milioni ya mirabaha kutoka MCSK, na PRISK licha ya kuwa na albamu 30. Nimepewa tu Shilingi 1295" - Kigame.

Muhtasari

• Reuben Kigame alilalamika  baada ya kupokezwa kiasi kidogo cha mrabaha licha ya ngoma zake kuwa na ushawishi mkubwa kutoka kwa rais, bendi za jeshi na hata vyama vya kisiasa.

Reuben Kigame aisuta PRISK, MCSK kwa mirabaha duni kwa wasanii.
Reuben Kigame aisuta PRISK, MCSK kwa mirabaha duni kwa wasanii.
Image: Facebook

Msanii wa injili ambaye pia ni alikuwa na nia ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka jana Reuben Kigame amemkaba shingoni rais Ruto baada ya Jumuiya ya Haki za Watumbuizaji Kenya, PRISK kumpa kiasi kidogo cha mirabaha licha ya nyimbo zake nyingi kuwa na ushawishi mkubwa nchini.

Kigame kupitia kurasa zake mitandaoni alionesha kutoridhishwa kwake baada ya kupokezwa shilingi 1295 kutoka PRIKS licha ya kudai kwamba nyimbo zake zinafagiliwa sana kote nchini kutoka kwa rais, bendi za jeshi na hata vyama vya kisiasa.

“Najua Makanisa yanapenda na kutumia muziki wangu na watu wa Kenya wamethamini kile ninachofanya kupitia utunzi wa nyimbo, na kwa hilo nabaki kushukuru kweli. Lakini kuna umuhimu gani wa kutoa nyimbo zinazopendwa na taifa hadi kufikia hatua ya Rais, Bendi za Jeshi na Polisi, vyama vya siasa, vyombo vya habari n.k kutumia nyimbo za namna hiyo ili wewe uishie kupewa 1295 kama mrabaha??” Kigame aliuliza kwa kuchukizwa.

Mtunzi huyo wa nyimbo alisema kuwa baada ya kupokea kiasi hicho finyu, haoni tena haja ya jumuiya ya PRISK kuendelea kuwepo kwa kile alisema kuwa haipiganii maslahi ya wasanii na watumbuizaji.

“Kwa nini PRISK iwepo ikiwa pesa nyingi zinazolipwa kwa wanamuziki zitaishia kufanya kazi za utawala na kutowanufaisha waundaji wa maudhui? Kwa nini si tu kuifuta?”

“Labda mimi ndiye tatizo. Labda mimi ni mdanganyifu tu, au ni rahisi sana kutumiwa, lakini nitasema moja kwa moja: Kufanya muziki nchini Kenya hakuna faida linapokuja suala la faida kwa wale wanaotaka kuifanya safi,” Alisema.

Mkosoaji huyo mkuu wa rais Kenyatta alizidi kumkoromea rais Ruto akimtaka kuwathamini na kuwalipa wasanii jinsi ambavyo anahaha na kubimbilika kushoto kulia kunadi miradi ya kimaendeleo.

“Najua watu hufikiria kuwa ninatania ninaposema sijawahi kutengeneza nusu milioni kupitia mrabaha wa muziki wangu kama ulivyolipwa na MCSK na PRISK katika maisha yangu na discography ya karibu albamu 30. Mheshimiwa Rais @WilliamsRuto, Ninawapa changamoto kuwa makini katika kuwalipa wanamuziki kama vile mlivyo makini kuhusu wakulima na miradi mingine,” alisema.