Mwanamke amuua jirani yake wa kiume kwa kushindwa kulipa bili ya umeme shilingi 59

Ugomvi baina ya wapangaji hao wawili ulijiri ambapo inadaiwa kuwa Adam aligoma kulipia deni la umeme ambao kwa kawaida wapangaji huchangia.

Muhtasari

• Kwa mujibu wa polisi, Brandina Fred alimchoma kisu kijana Erick Adam mwenye umri wa miaka 32.

• Kamanda Masejo alisema, Jeshi hilo bado linamshikilia kwa mahojiano, mtuhumiwa huyo na bado anahojiwa kuhusiana na tuhuma hizo.

Mwanamke mjamzito apatikana amedungwa visu mgongoni
Mwanamke mjamzito apatikana amedungwa visu mgongoni
Image: Maktaba//The Star

Jeshi la polisi katika mkoa wa Arusha nchini Tanzania linachunguza kisa ambapo mwanamke mmoja mpangaji alimuuwa kijana mpangaji mwenzake jirani kwa kushindwa kulipa bili ya umeme ambayo ilitajwa kuwa shilingi elfu moja ambacho ni kiasi sawa na shilingi 59 pekee za Kenya.

Kwa mujibu wa polisi, Brandina Fred alimchoma kisu kijana Erick Adam mwenye umri wa miaka 32 kutokana na kushindwa kumudu mchango wa kulipia bili ya umeme wa vyumba hivyo vya kupangisha.

Tukio hilo limetokea mapema wiki hii baada ya kutokea ugomvi baina ya wapangaji hao wawili ambapo inadaiwa kuwa Adam aligoma kulipia deni la umeme ambao kwa kawaida wapangaji huchangia.

Kamanda wa polisi mkoa Arusha, Justine Masejo ambaye alizungumza na jarida la Mwananchi alisema tukio hilo lilitokea nyakati za mchana, Brandina akiwa na kisu akijiandaa kwa mapishi ya chakula cha mchana.

"Kilichotokea ni kuwa wote ni wapangaji walikuwa wakigombana huyu binti alikuwa na kisu kwa kuwa alikuwa jikoni, sasa ndio alimchoma mwenzake," alisema kama alivyonukuliwa na jarida hilo.

Amesema Adam alifariki kutokana na kutokwa na damu nyingi baada ya kuchomwa kisu.

Kamanda Masejo alisema, Jeshi hilo bado linamshikilia kwa mahojiano, mtuhumiwa huyo na bado anahojiwa kuhusiana na tuhuma hizo.

"Taratibu zikikamilika atafikishwa mahakamani kutokana na tuhuma ambazo zinamkabili," amesema kamanda huyo, na kwamba mwili wa Adam umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mountmeru kwa uchunguzi zaidi.