Ferdinand Omanyala afichua hajapokea shilingi milioni 2 alizoahidiwa na rais Ruto

“Haijaingia kwa akaunti yangu bado," Omanyala alisema.

Muhtasari

• Omanyala aliweka wazi kuwa pesa alizoahidiwa bado hazijaingia kwenye akaunti yake ya benki wiki mbiii baada ya ahadi hiyo kutolewa.

• Serikali ilimtunuku Fedinand shilingi milioni mbili baada ya kumuomba Rais ‘chai’ alipoalikwa kuzungumzia mashindano aliyoyashiriki.

akishiriki mashindano ya dunia huko Oregon
Bingwa wa Afrika katika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala akishiriki mashindano ya dunia huko Oregon
Image: TWITTER// FERDINAND OMANYALA

Mshikilizi wa rekodi ya Afrika katika mbio za mita 100 na bingwa wa mbio hizo wa Jumuiya ya Madola Ferdinand Omanyala amefichua kuwa bado hajapokea zawadi ya shilingi milioni 2 aliyoahidiwa na Rais William Ruto.

Akizungumza wakati wa mahojiano na kituo cha runinga cha Look Up, Omanyala aliweka wazi kuwa pesa alizoahidiwa bado hazijaingia kwenye akaunti yake ya benki wiki mbiii baada ya ahadi hiyo kutolewa.

“Haijaingia kwa akaunti yangu bado” alisema mwanariadha huyo.

Siku ya Jumanne tarehe 13 mwezi Juni, Serikali ya Kenya ikiongozwa na Rais William Ruto iliwazawadi Ferdinand na bingwa wa mbio za mita 1,500 Faith Kipyegon kwa ubabe wao katika mashindano ya Diamond League.

Serikali ilimtunuku Fedinand shilingi milioni mbili baada ya kumuomba Rais ‘chai’ alipoalikwa kuzungumzia mashindano aliyoyashiriki.

"Nina ombi mbili pekee yake tu Bwana Rais. Ninafanya mazoezi yangu katika uwanja wa Kasarani na uwanja wa kufanyia mazoezi imechanika kabisa… na pia sisi kama wanaridha tunataka kutoka hapa na chai."

Omanyala katika hotuba hiyo hiyo alimuahidi Rais kuwa ndani ya miezi miwili ataweza kunyakuwa medali katika mashidano ya dunia, kitu ambacho hakijawahi kushudiwa hapo mbeleni mwanariadha kutoka Afrika kushinda medali yoyote katika mashindano hayo.

Serikali pia ilimtunuku Faith Kipyegon  shilingi Milioni tano pesa taslimu na nyumba yenye thamani ya shilingi Milioni 6 kwa kuvunja rekodi mbili za dunia ndani ya wiki moja.

Rais alisema kuwa hii itakuwa zawadi kwa rekodi mbili alizovunja katika wa mita 5,000 na mita 1,500.

"Ameshinda na kuvunja rekodi mbili za dunia za mita 1500 huko Florence Italy na ya mita 5000 mjini Paris, Ufaransa. Serikali ya Kenya inakwenda kumzawadia jumla ya Shilingi milioni 5 kwa rekodi moja na tutampa nyumba yenye thamani ya Shilingi milioni 6 kwa rekodi nyingine," Ruto alisema.