UCHUMI WA NCHI

Uhuru Kenyatta lazima amheshimu Rais Ruto - Moses Kuria

Anafaa akubali kuwa Ruto alishinda uchaguzi, Nchi hii kubwa kuliko yeye

Muhtasari

•Kuria, amekuwa akimsuta sana kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga kwa kuendesha maandamano, kile ambacho alidai kuwa nia yake ni kulemeza uchumi na ustawi wa taifa.


Image: Moses Kuria//TWITTER

Waziri wa biashara nchini Moses Kuria amedakia kuwa rais mstaafu Uhuru Kenyatta aheshimu uongozi wa serikali ya Rais William Ruto.

Kuria amesema hilo alipokuwa amehudhuria hafla ya uzinduzi wa albamu mpya ya mwanamuziki Ngaruiya Junior maarufu King of Kigooco katika uwanja wa Gatundu kaunti ya Kiambu, Julai 9.

“Bwana Uhuru Kenyatta lazima amheshimu Rais William Ruto na akubali kuwa alishinda uchaguzi. Nchi hii ni kubwa kuliko Uhuru na maslahi yake ya kibinafsi.Binafsi nitaitetea na kuilinda Serikali hii kama nilivyomfanyia mwenzangu wa jimbo wakati alipokuwa Rais. Mkoa wa Mt Kenya ni mbia mkubwa na kwa manufaa ya serikali hii na hatutaukubali upuuzi tena.Niliungana na viongozi wenzangu na mashabiki wa mwanamuziki wetu mkubwa Ngaruiya Junior 'King Of Kigooco' kama mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa albamu yake, katika uwanja wa Gatundu kaunti ya Kiambu,” Kuria aliposti katika mtandao wake wa Twitter.

Haya yanajiri wakati ambapo baadhi ya viongozi serikalini wakihisi kuwa, mpango wa maandamano unaoendeshwa na viongozi wa upinzani kulalamikia hali ngumu ya maisha unafadhaliwa na rais mstaafu.

Waziri Kuria amekuwa akigonga vichwa vya habari, hasa baada ya uvumbuzi wa sakata ya mafuta ya kupikia, ambayo inadaiwa kuwa alihusika kwa kiwango kikubwa ambayo ingeelekeza nchi kupoteza karibu shilingi bilioni 10.

Kuria, amekuwa akimsuta sana kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga kwa kuendesha maandamano, kile ambacho alidai kuwa nia yake ni kulemaza uchumi na ustawi wa taifa.