MAANDAMANO YENYE UTATA

Maandamano yanayopangwa Jumatano na Azimio hayatafanyika - Ruto

Mimi nataka nikuhakikishie Raila Odinga, niko nawe macho kwa macho na tutakutana siku hiyo - Ruto

Muhtasari

•Bwana kitendawili alileta fujo, akaleta mapindizi watu wakakufa miaka ya hapo nyuma. Alimsumbua Mzee Kibaki sana pia.

RAIS WILLIAM RUTO
Image: TWITTER

Rais William Ruto amekiri kwamba maandamano yanayopangwa na Azimio la Umoja Jumatano wiki ijayo hayatafanyika.

Ruto ameeleza kuwa ni kutokana na maandamano ya siku zilizopita ambapo watu waliaga dunia na wengine kupata majeraha mabaya huku mali yasiyokadirika yakiharibiwa na waandamanaji, ambapo alisema huwa hataruhusu hilo liendelee tena.

Mliona juzi, walifanya maandamano Ijumaa iliyopita ile ingine watu saba wakakufa, wamefanya maandamano juzi watu nane wamekufa. Mimi nataka niwaulize, mnataka tuendelee na hii maandamano? Mnataka tuendelee na hii maandamano? Mimi nataka niwaambie, maandamano haiwezi kufanyika tena katika taifa la Kenya,”  Aliuliza Ruto.

Rais aliendelea kumkashifu vikali kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga, ambapo alisema kuwa alileta fujo, mapinduzi yaliyosababisha vifo vya watu miaka iliyopita, ambapo aliapa kuwa maandamano wanayopanga kufanya kamwe hataruhusu yafanyike.

Wacheni niwaambie, bwana kitendawili alileta fujo, akalete mapinduzi watu wakakufa miaka ya hapo nyuma. Akakuja na kumhangaisha Mzee Kibaki; mara choo, mara carpet...Kibaki akafanya kazi lakini hakufanya kama ilivyotakikana kufanyika. Bwana Raila Odinga nataka nikuambie uchaguzi uliisha,” Aliendelea.

Haya yanajiri wakati ambapo muungano wa Azimio umetoa taarifa inayorekebisha kalenda ya maandamano, ambapo walisema kuwa wiki ijayo Jumatano maandamano yatakuwa ya siku tatu mfululizo kutoka Jumatano hadi Ijumaa.

Muungano huo uliotoa taarifa hiyo kile ambacho walidai kuwa ni kutokana na maoni na malalamishi waliyopokea kutoka kwa umma, wakitaka maandamano ya kupinga gharama ya juu ya maisha kuendelea hadi pale serikali itakapowasikia.