CS Kuria azua minong'ono mitandaoni kwa ujumbe wenye ukakasi kuhusu kifo

Ujumbe wa Kuria unakuja wakati ambapo kila mrengo unasimama vikali na kujipiga kifua kuhusu mustakabali wa maandamano ya siku ya Jumatano Julai 19.

Muhtasari

• Kutokana na kauli hii, baadhi wanahisi Kuria huenda alikuwa anarejelea maandamano na kuyapa uhai kwamba yatatibuliwa na kusambaratishwa.

CS Kuria atoa kauli ya ukakasi kuhusu maandamano ya Jumatano.
MAANDAMANO CS Kuria atoa kauli ya ukakasi kuhusu maandamano ya Jumatano.
Image: Twitter

Waziri wa viwanda na biashara Moses Kuria amezua mtafaruku miongoni mwa Wakenya mitandaoni baada ya kutoa ujumbe wa kumtabiria mtu asiyejulikana kifo.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Kuria aliandika ujumbe mfupi uliojaa maana fiche tumbi nzima akisema kuwa mtu huyo atakufa Jumatano wiki hii na kuzikwa wiki moja baadae na mambo yake kusahaulika.

Atakufa Wednesday 19th azikiwe Saturday 29th. Jowi !” Moses Kuria aliandika na kuwaacha Wakenya wakikuna vichwa wasiweze kupata majibu sahihi kuhusu aliyekuwa akimaanisha katika ujumbe huu wenye ukakasi mwingi.

Baadhi walihisi kwamba huenda kuna kitu Kuria anajua na ambacho ameamua kukiweka wazi kwa Wakenya kupitia ujumbe fiche na wengine walihisi mbunge huyo wa zamani wa Gatundu Kusini alikuwa anajaribu kuhaisha maandamano ya kuyarejelea kama mtu.

Ikumbkwe hiyo Jumatano ya tarehe 19 ambayo Kuria anarejelea kwenye ujumbe wake ndio siku ambayo muungano wa Azimio umetangaza duru ya tatu ya maandamano yao makubwa kote nchini, licha ya rais Ruto kutoa kali kali kwamba hakuna maandamano ambayo yatafanyika siku hiyo.

Kutokana na kauli hii, baadhi wanahisi Kuria huenda alikuwa anarejelea maandamano na kuyapa uhai kwamba yatatibuliwa na kusambaratishwa kabisa siku hiyo, yasiwahi tokea tena nchini.

“Hili likitoka kwa mtu aliyekaribia kufa kwa kuchomeka miguu na makaa, aliyekaa hospitalini kwa miezi kadhaa, aliomba dua zetu na rehema za Mungu…. Enyewe binadamu husahau. Ni watu kama wewe kumshauri Rais vibaya. Watu kama wewe hawafai kuwa na nafasi nchini Kenya,” Anwar Saddat alimwambia.

“Lakini alisema nani? Kwa nini sisi sote tunafanyiwa kazi?” Abraham Mutai alionekana kusimama upande wake.

Maoni yako ni yepi kuhusu kauli hii ya Kuria?