Isiolo yajiondoa katika mpango wa maandamano, wamtaka Odinga kustaafu siasa

Akizungumza mjini Isiolo wikendi gavana Abdi Hassan Guyo alisema kuwa maandamano hayo ya kila wiki pia yanazorotesha uchumi wa nchi wakati ambapo serikali inajaribu kuuimarisha.

Muhtasari

• "Hapa Isiolo, hatutafanya maandamano. Tulisema sisi wakaaji wa Isiolo hatuna urafiki na maandamano." - Guyo asema.

• Guyo aliutaka uongozi wa Azimio kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na gharama ya juu ya maisha badala ya maandamano.

gavana wa Isiolo amtaka Odinga kustaafu siasa.
MAANDAMANO gavana wa Isiolo amtaka Odinga kustaafu siasa.
Image: Facebook

Gavana wa Isiolo Abdi Hassan Guyo amemtaka Kiongozi wa Azimio La Umoja Raila Odinga kusitisha maandamano dhidi ya serikali.

Guyo alisema kuwa uharibifu kutoka kwa maandamano hayo unachangia gharama kubwa ya maisha kutokana na upotevu wa fedha na uharibifu wa mali.

Akizungumza mjini Isiolo wikendi Guyo alisema kuwa maandamano hayo ya kila wiki pia yanazorotesha uchumi wa nchi wakati ambapo serikali inajaribu kuuimarisha.

"Maandamano sio suluhisho la gharama kubwa ya maisha," alisema.

Guyo aliutaka uongozi wa Azimio kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na gharama ya juu ya maisha badala ya maandamano.

"Hapa Isiolo, hatutafanya maandamano. Tulisema sisi wakaaji wa Isiolo hatuna urafiki na maandamano. Tuna nafasi tu ya matukio yanayohusiana na maendeleo," aliongeza.

Gavana huyo licha ya kukiri kuwa gharama ya maisha imepanda, hata hivyo alisema kuwa mandamano haikuwa suluhu.

Aidha mkuu huyo wa Kaunti alimtaka Raila kustaafu siasa na kuacha serikali ya siku hiyo iwafanyie kazi Wakenya.

"Ninamwomba Raila kwa sababu tulimsaidia kutafuta kura, lakini akakataliwa. Sasa anafaa kustaafu na kuiacha serikali ifanye kazi," Guyo aliongeza.

MCA huyo wa zamani wa Matopeni pia aliambia Upinzani kuipa Kenya Kwanza muda wa kufanya kazi.

Guyo alisema kuwa Rais William Ruto anafaa kupewa muda wa kutoa manifesto yake.

“Nataka kumwambia Raila Odinga kuipa serikali muda wa kufanya kazi katika miaka mitano ijayo, kisha uje kumkosoa rais kwa ahadi ambazo hakutimiza,” akasema.

Guyo ni miongoni mwa viongozi wa Isiolo waliojiunga na chama cha United Democratic Alliance hivi majuzi.

Gavana huyo alisema yuko tayari kwa uchaguzi mdogo baada ya kukihama chama cha Jubilee.

Guyo alikuwa Gavana pekee wa Jubilee aliyechaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.