Vijana Kibera wamtaka Odinga kusitisha maandamano,"Tunakupigania na hatujui ajenda zako!"

"Sasa hivi hali ya uchumi iko juu na si eti ni lawama kwa mtu yeyote. Sasa hivi dunia yote kila kitu iko juu na si Kenya peke yake." - Odhiambo Owino alisema.

Muhtasari

• "Mtu mwenye tunapigania hata hatujui ajenda zake. Yeye anasema stori ya seva na ukinagalia hiyo stori kura zilipigwa lini? " - Owino aliwauliza vijana.

Vijana Kibera wamemtaka Odinga kusitisha maandamano.
Vijana Kibera wamemtaka Odinga kusitisha maandamano.
Image: Screengrab

Vijana katika mtaa wa mabanda wa Kibera jijini Nairobi wametoa wito na ombi kwa kinara wa Azimio Raila Odinga kusitisha maandamno ya sku tatu ambayo yameng’oa nanga mapema Jumatano.

Vijana hao wakiongozwa na kiongozi wa vijana KIbera Odhiambo Owino, walitoa wito kwa Odinga kusitisha maandamano hayo kwa kusema kwamba yatalemaza biashara zao.

Owino alisema kuwa gharama ya maisha kuwa juu si lawama kwa mtu yeyote hata serikali bali ni mfumko ambao umeshuhudiwa katika mataifa mengi duniani.

“Kwa siku ya leo unaona hivyo wamepanga ni maandamano ya siku tatu, lakini sisi wana Kibera ndio tunaumia san asana hii ghetto yetu. Sasa hivi hali ya uchumi iko juu na si eti ni lawama kwa mtu yeyote. Sasa hivi dunia yote kila kitu iko juu na si Kenya peke yake. Kwa hiyo hii mambo ya maandamano yanatuathiri hata Zaidi, yanaturudisha sifuri,” alisema Owino.

Owino aliwataka vijana wenzake kuwa mabalozi wa Amani akisema kuwa kuumizana hakuna faida yoyote kupigania wanasiasa.

“Sasa hivi vijana tunajiingiza kwenye maandamano ambayo si ya Amani. Mtu mwenye tunapigania hata hatujui ajenda zake. Yeye anasema stori ya seva na ukinagalia hiyo stori kura zilipigwa lini? Sisi tunakuwa tu tunatumika halafu kuna mtu ako na matakwa ya kibinafsi, unaona,” alisema Owino.

Kiongozi huyo wa vijana alisema kuwa viongozi ndio huleta shida kwenye mitaa duni huku hali kama hizo haziwezi shuhudiwa katika mitaa ya kifahari.

Vijana hao walisema kuwa tayari wamezima moto uliokuwa umewashwa kwenye barabara wakisema kuwa wamesha amua hakuna mambo ya maandamano Kibera.