Malala adai kuwa Azimio wanapanga fujo Jumatano usiku

Mnaweza mkaenda kanisani, au katika boma za waathiriwa, ila mkutano usiku tunawaona sana - Malala

Muhtasari

• Muungano wa Azimio ulitangaza mkutano wa Jumatano usiku kwa kuwasha mishumaa ili kuomboleza watu waliofariki kwa maandamano yaliyopita.

Katibu mkuu wa UDA Cleophas Malala
Katibu mkuu wa UDA Cleophas Malala
Image: Facebook

Katibu mkuu wa chama cha UDA Cleophas Malala ameshutumu muungano wa Azimio la Umoja kwa kuhairisha maandamano ya Jumatano kama yalivyopangwa na viongozi hao na kusema pia ni njama ya kuleta usiku.

Mkuu huyo wa UDA amedai kuwa kuhairishwa kwa maandamano hayo ili watu waungane kuomboleza kwa kuwasha mishumaa patachipuka fujo ambazo huenda zitachangia utovu wa usalama katika taifa.

Tunajua mpango wenu, kwamba mmehairisha maandamano ya Jumatano, na mkasema kwamba watu wakusanyike na wawashe mishumaa usiku, sisi tunataka tuwaambie kwamba tunajua kuwa mnataka kuleta fujo usiku, na mtu yeyote ambaye ataleta uhalifu usiku tunamwambia kwamba Rais wetu ameana amri kwamba ni lazima kuwe na usalama usiku,” alisema Malala.

Kiongozi huyo pia alielekeza shutuma zake kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kile ambacho alidai kuwa maandamano yanayofanywa na mrengo wa Azimio yanafadhiliwa kwa kiasi kikubwa naye, ambapo alimrai awache kuyafadhili maandamano hayo.

Tunaomba Rais wetu mstaafu Uhuru Kenyatta aache kufadhili maandamano ya muungano wa Azimio la Umoja na badala yake amruhusu Rais wetu aweze kutimiza ahadi alizowaahidi Wakenya wakati wa Kampeni,” alisihi Malala.

Malala alieleza kuwa Azimio wanajificha kwa kutumia kuomboleza na kwa kupanga kuwasha mishumaa usiku, ambapo alishauri upande huo wa upinzani kuwa kuna pahali mwafaka pa kufanyia hivyo hasa katika sehemu za kuabudu.

Wacheni kujificha kuwa mnaomboleza kwa wale ambao walifariki, sisi sote tunaomboleza, na kuna njia ambazo maombolezi yanafaa kufanyika. Mnaweza enda kanisani, muende mkaomboleze muombee familia zile, mnaweza enda katika boma za wale walioathirika na muombe pamoja, lakini kusema kwamba usiku mnataka kuwasha mishumaa mnataka kujificha, mfanye uhalifu,” aliendelea.

Haya yanajiri wakati ambapo muungano wa Azimio la Umoja ulitoa taarifa hapo jana ukitangaza kuhairisha maandamano yao kwa ajili ya kupisha shughuli za uombolezaji kwa watu waliofariki katika maandamano yaliyopita.