Ushuru tunaotozwa ni kama kutafuta damu kwa nzi - Jeremiah Kioni

Alisema akiweka Biblia chini kila kitu kitashuka, bado Biblia iko juu? Kimeturamba - Kioni

Muhtasari

•Mwandani huyo wa Azimio alisema kuwa bado wana nafasi nzuri ya kubadili mustakabali wa taifa na kuinua uchumi 2027.

Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee Jeremiah Kioni
Image: Jeremiah Kioni /TWITTER

Aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni ameikashifu serikali ya Kenya Kwanza kuhusu gharama ya juu ya maisha na kushindwa kukidhi mahitaji ya Wakenya kama walivyoahidi wakati wa kampeni.

Katika mahojiano na Radio Jambo Julai 25, Kioni alisisitiza kuwa Rais William Ruto aliwahadaa Wakenya wakati wa kampeni na hivyo kujizolea ushindi wakati huo ambapo alisema kuwa ni wakati wake sasa kung’atuka mamlakani.

“William Ruto aliwahadaa Wakenya, alisema wakati wa kampeni kuwa ni ushirikiano wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga ndio ulifanya kila kitu kikapanda juu, alisema akiweka Biblia chini kila kitu kitashuka hasa bei ya unga, kwani bado hiyo Biblia iko juu?” aliuliza Kioni.

Kiongozi huyo wa Jubilee pia aliulinganisha uchumi enzi za Moi wakati Kibaki aliingia mamlakani na wakati wa sasa ambapo Ruto ameingia katika uongozi wa taifa na kusema kuwa Kibaki alikuwa na mikakati ila ya Ruto ni hadaa tu hana mipango.

“Wakati wa Kibaki alipata uchumi umeharibika kwa kiasi kikubwa sana. Kibaki alianza zero na alipoingia katika uongozi cha kwanza alisema kuwa ni watoto waende shule, hakusema anangoja mswada wowote wa fedha, kinyume cha Rais wa sasa ambaye anawatoza Wakenya ushuru kwa madai ya kutaka kuboresha uchumi,” Aliendelea.

Haya yanajiri wakati ambapo muungano wa Azimio la Umoja umehairisha maandamano yao yaliyopangwa kufanyika Jumatano wiki hii kwa ajili ya kuandaa maombolezi juu ya wale waliofariki katika maandamano yaliyofanyika siku tatu mfululizo wiki jana.

Kulingana na Kioni, anadai kuwa bado wana mpango wa kuliongoza taifa ambapo alisema kuwa wafuasi wao wasiwe na shaka kwa kuwa bado wapo katika nafasi nzuri ya kuyabadili yale mbayo yanawakabili.

Mwanachama huyo ya Jubilee alisema kuwa wamejipanga kulingana na katiba ya taifa kuwa mwaka wa 2027 wana matumaini ya kujaribu tena iwapo watakaidi kipengele cha 1 cha katiba ambacho kinadokeza kuwa uongozi wa taifa upo miongoni mwa wananchi.