Rafiki yangu Raila, mimi niko tayari kuzungumza ana kwa ana na wewe - rais Ruto

"Kama ulivyokuwa ukijua, ninapatikana kukutana nawe mmoja mmoja wakati wowote kwa urahisi,” Ruto alimjibu Odinga.

Muhtasari

• Hata hivyo, madai ya Odinga kwamba rais Hassan alirudi baada ya kushindwa kuwakutanisha hayajadhibitishwa na ikulu ya Dodoma.

Ruto na Raila waonesha nia ya kupatana.
HANDSHAKE Ruto na Raila waonesha nia ya kupatana.
Image: Facebook

Siku moja baada ya kinara wa ODM na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kutoa kile kilichochukuliwa kama ufichuzi wa kile kinachoendelea nyuma ya pazia baina yake ya rais Ruto, mkuu wa taifa ametoa naye tamko lake vile vile.

Ikumbukwe Jumanne katika mkutano na vyombo vya habari vya kimataifa, Odinga alifichua kwamba wiki mbili zilizopita rais Ruto alimwalika rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuja nchini ili kuwapatanisha naye.

Odinga alimlaumu Ruto kwamba licha ya kumwalika Hassan, rais huyo alifika na kukaa kwenye hoteli kwa siku mbili bila kuonana nao na akaamua kurudi nchini kwake na hivyo kupatana kwa wababe hao wa siasa za humu nchini kufeli kwa mara nyingine.

“Rais wa Tanzania [Samia Suluhu] alikuwa nchini (Kenya)wiki mbili zilizopita. Ilikuwa ni kwa mwaliko wa [Rais] Ruto. Alibaki akisubiri. Tulikuwa tayari, lakini wao [Kenya Kwanza] hawakupatikana. Kwa kweli, ilimbidi kukaa huku kwa mbili,” Raila aliambia wanahabari.

Ruto katika tamko lake ambalo lilionekana kama jibu kwa madai ya Odinga ambayo hata hivyo hayajadhibitishwa na ikulu ya Dodoma, alisema kwamba yuko nje ya nchi na atakaporejea yuko tayari kabisa kufanya mazungumzo ya uso kwa uso kwa kiongozi wa upinzani muda wowote.

Kupitia ukurasa wa Twitter, Ruto aliandika hayo akimtaja Raila kama ‘rafiki yangu’.

“Rafiki yangu @RailaOdinga, nimeenda Tanzania kwa mkutano wa rasilimali watu ili kuoanisha upanuzi wa fursa za ajira katika bara letu. Nitarudi kesho jioni, na kama ulivyokuwa ukijua, ninapatikana kukutana nawe mmoja mmoja wakati wowote kwa urahisi,” Ruto alijibu.

Tako hili la Ruto linakuja siku mbili baada ya mrengo wa Azimio kupiga breki maandamano yaliyokuwa yameratibiwa Jumatano leo hii katika mwendelezo wa maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika tangu wiki juzi.

Je, huu ni mwanga wa kuelekea katika upatanishi wa Amani?