Raila ajigamba kupata saini milioni 8 na kupita kura milioni 7.1 alizopata Ruto

Kufikia sasa kulingana na tovuti ya Tumechoka.com, Azimio wamekusanya saini za Wakenya milioni 8.5 ikiwa ni chini ya wiki mbili tu tangu kuanzishwa kwa vuguvugu hilo.

Muhtasari

• “Bw Ruto kulingana na Chebukati alipata kura milioni 7.1, tayari tuna sahihi zaidi ya milioni 8,” Odinga alijitapa.

Raila ampiga dongo Ruto kuhusu saini za wapiga kura.
Raila ampiga dongo Ruto kuhusu saini za wapiga kura.
Image: TWITTER

Kinara wa upinzani Raila Odinga ameonesha furaha yake baada ya kupata saini za Wakenya Zaidi ya milioni 8 katika vuguvugu alilolianzisha la Tumechoka.com kukusanya saini ili kumbandua rais Ruto mamlakani.

Kupitia Twitter yake, Odinga alionesha furaha hiyo akipakia picha ya skrini ya tovuti ya tumechoka.com ikionesha Zaidi ya saini milioni 8 zilizokusanywa kufikia sasa, ikiwa ni chini ya wiki mbili tu tangu kuzindua vuguvugu hilo.

Odinga wakati huo huo pia alitupa dongo kwa rais Ruto akisema kwamba amekusanya saini ambazo zimepita kura alizotangazwa kushinda nazo uchaguzi wa mwaka jana, milioni 7.1

“Bw Ruto kulingana na Chebukati alipata kura milioni 7.1, tayari tuna sahihi zaidi ya milioni 8,” Odinga alijitapa.

Katika picha hiyo, Odinga alionesha kukusanya saini za Wakenya milioni 8.5 ambao anasema wamepoteza matumaini na serikali ya Kenya Kwanza na wanataka rais Ruto kubanduliwa mamlakani.

Hii inawiana na takwimu za utafiti uliofanyika mapema wiki hii ukionesha asilimia kubwa ya Wakenya wakiwa wamepoteza matumaini na serikali ya Kenya kwanza.

Odinga hata hivyo hakudokeza iwapo mchakato wa kukusanya saini utakamilika muda gani.

Awali, Azimio walikuwa wamesema walikuwa wanalenga kupata saini za Wakenya milioni kumi, wakiendeleza maandamano yao ya kupinga uongozi wa bwana Ruto, Odinga akishikilia msimamo kwamba hakushindwa uchaguzi wa mwaka jana bali ni ukarabati wa takwimu ulifanywa na tume husika ikiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti Wafula Chebukati.