Ruto awataka Raila na Uhuru kuomba msamaha kwa kufadhili maandamano

Rais alitaja kama mzaha machozi ya viongozi hao waliokongamana katika ibada ya kuwakumbuka waliopoteza maisha, akisema kwamba wasingefadhili na kuandaa maandamano, watu hawangefariki.

Muhtasari

"Na kusonga mbele natumai sisi wote tumejifunza athari hasi zinazokuja na kuandaa maandamano,” alisema Ruto.

• Ruto alisisitiza kwamba polisi hawatotishwa katika kutekeleza wajibu wao wa kulinda maisha na mali ya mwananchi.

Ruto awataka Odinga na Kenyatta kuomba msamaha
Ruto awataka Odinga na Kenyatta kuomba msamaha
Image: Facebook, Maktaba

Rais William Ruto amewataka viongozi wa upinzani kuomba taifa msamaha kwa kuandaa maandamano ambayo yalisababisha makumi ya watu kufariki katika matukio mbali mbali lakini pia kuharibiwa kwa mali yenye thamani isiyokadirika na taifa kupoteza mabilioni ya pesa kupitia ushuru baada ya biashara nyingi kulemzwa.

Akizungumza katika kaunti ya Kilifi alikoongoza hafla ya kukabidhiwa rasmi kwa vitambulisho na vyeti vya kuzaliwa vya watu wa jamii ya Wapemba waliojumuishwa rasmi kama Wakenya, Ruto alisema kuwa ni unafiki kuona viongozi wa upinzani wakikusanyika kuchangisha pesa kuwasaidia walioathirika na maandamano hayo wakati wao ndio waliyapanga.

Ruto alisema kwamba viongozi hao wakiongozwa na Raila Odinga na Uhuru Kenyatta hawakuwa wakweli katika kuomboleza waliofariki kwa maandamano ambayo wao wenyewe waliandaa.

“Na watu ambao wako nyuma ya haya maandamano, watu ambao ndio wanafadhili na kupanga haya machafuko ambayo yamesababisha kupotea kwa maisha ya vijana wa Kenya, kuharibiwa kwa biashara za watu, mali ya umma, watu kama hao wanafaa kujionea aibu wenyewe,” rais Ruto alisema.

“Wanafaa kuomba msamaha kwa watu wa Kenya. Kama si wao kufadhili machafuko, hatungepoteza maisha, biashara na mali ya umma. Na kusonga mbele natumai sisi wote tumejifunza athari hasi zinazokuja na kuandaa maandamano,” aliongeza.

Kiongozi huyo wa taifa alisisitiza kwamba maafisa wa polisi hawatotishiwa katika kutekeleza wajibu wao wa kulinda maisha na mali ya mwananchi wa kawaida dhidi ya mashambulizi ya waandamanaji.

“Hatutakuwa tunaendeleza utamaduni wa machafuko. Hatutavumilia kuharibiwa kwa maisha, biashara na mali ya watu kwa kisingizio cha kumenyana kisiasa, hilo halitokuwa kati yetu,” alisema.

Ruto alisema haya wakati viongozi wa upinzani wakikongamana katika boma la Kalonzo Musyoka mtaani Karen katika hafla ya kuwakumbuka wale waliopoteza maisha kwenye machafuko yaliyoshuhudiwa wiki jana wakati wa maandamano ya kupinga serikali.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Odinga, Kenyatta miongoni wa viongozi wengine wa upinzani, waliweza kuchangisha Zaidi za shilingi milioni 4.5 ambazo Musyoka alisema zitakwenda katika kuzisaidia zile familia za waandamanaji waliopoteza maisha lakini pia kugharamia mahitaji mbali mbali ya wale walioko katika hospitali mbali mbali nchini.