Wanawake kaunti ya Murang'a wageukia biashara ya kununua mbegu za kiume

Wanawake hao wananunua mbegu za kiume kwa sh300,000 kutoka kwa wanaume umri kati ya 20-40 ambao ni warefu na walio na rangi ya ngozi ya wastani, yaani si weupe sana na si weusi kupindukia.

Muhtasari

• Mwanamke mmoja mjini humo ameambia Taifa Leo kwamba siku hizi wanawake walioamua kushikilia uhuru wao wa kimaisha hawataki kutafuta ndoa.

Mwanamke mjamzito
Mwanamke mjamzito
Image: maktaba

Kutokana na hali ya ulevi kwa wanaume iliyokithiri katika eneo pala na Mlima Kenya, gazeti la Taifa Leo limefichua kwamba sasa wanawake katika kaunti ya Murang’a wamelazimika kununua mbegu za kiume kutoka kwa wanaume wa nje ili angalau kupata mimba – kwani wanaume wao hawana uwezo wa kuweza kuwapachika mimba kutokana na kufyonzwa nguvu kwa makali ya vileo haramu.

Gazeti hilo linaripoti kwamba wanawake katika kaunti hiyo sasa wapo radhi kumlipa mwanamume hadi kiasi cha shilingi laki 3 ili tu kuwapachika mimba.

Wanaume wanaopendelewa zaidi katika biashara hiyo ni walio na umri wa kati ya miaka 20 hadi 40 lakini wawe wako katika kozi ambazo wanawake hao – Miss Independents – wanaziona ni za watu werevu,” Taifa Leo walibaini.

Aidha, wanawake wengi wamesema wanapendelea wanaume warefu na walio na rangi ya ngozi ya wastani, yaani si weupe sana na si weusi kupindukia.

Mwanamke mmoja mjini humo ameambia Taifa Leo kwamba siku hizi wanawake walioamua kushikilia uhuru wao wa kimaisha hawataki kutafuta ndoa na badala yake “sisi tuna tu mbegu ili tuzae natafuta kizazi”.

“Lakini katika kuzaa, tunafuatilia sana bahati ya kuwa na watoto wenye sura za kupendeza na pia ubongo stadi wawezesha kung’ara masomoni,” amesema mwanamke huyo ambaye kulingana na ripoti hiyo hakutaka kutambuliwa kwa jina.

Katika hali hiyo, mwanamke aliye katika maamuzi hayo na amefikia awamu ya kusaka mimba anatumana kazi ya kutafutiwa ‘kidume cha mbegu’.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 38 kwa sasa, alimlipa kijana wa umri wa miaka 23 ambaye ni mwanafunzi wa taaluma ya udaktari na ambaye anasomea katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Alimlipa Sh300,000.

“Lakini alipopata habari kuwa nimepata pacha alianza kunidai Sh300,000 za ziada lakini nikamweleza hatukuwa tunauziana watoto bali kazi yake ilikuwa ya kuuza uwezo wa kutunga mimba bila kujali kama ningezaa mtoto mmoja au hata watoto 50 kwa mpigo mmoja,” aliambia Taifa Leo.