Wahudumu wa mochwari mahakamani baada ya panya kula maiti ya mtoto

Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi wa maiti ya kitoto hicho kichanga, majeraha yalipatikana kichwani ambayo yalibainishwa kuwa ni kutokana na kudonwa na mnyama aina ya panya.

Muhtasari

• Hudumu yeyote atakayepatikana akizembea katika jukumu lake atasimamishwa kazi mara moja.

Chumba cha kuhifadhi maiti
Chumba cha kuhifadhi maiti
Image: BBC

Wahudumu wa mochwari moja nchini Uganda huenda wakajipata matatani baada ya kudaiwa kuzembea kazini na kuacha panya kula maiti ya mtoto.

Kwa mujibu wa ripoti ya jarida la Daily Monitor, uchunguzi wa maiti uliotolewa na polisi wiki jana ulibaini kwamba maiti ya kitoto kichanga iliyokuwa imehifadhiwa katika mochwari ya Kawempe jijini Kampala ilikuwa imeliwa na panya.

Msemaji wa polisi jijini Kampala Patrick Onyango aliambia jarida hilo kwamba kitoto hicho kichanga kilifariki katika hospitali hiyo na uchunguzi wa maiti ulibaini kililiwa na panya kikiwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali hiyo.

“Jeraha la kichwani lilitokana na kudonwa kwa panya. Hili ni baada ya kifo cha mtoto. Uongozi wa mochwari hii huenda ukashtakiwa kwa kuzembea kazini,” Onyango alisema kama alivyonukuliwa na gazeti hilo.

Kwa mujibu wa kanuni zilizotolewa na baraza linalosimamia wahudumu wa afya nchini humo, mhudumu yeyote atakayepatikana akizembea katika jukumu lake atasimamishwa kazi mara moja.

Hata hivyo, gazeti hilo lilisema kwamba mpaka wakati ripiti hiyo ilikuwa inachapishwa, bado hakukuwa na mhudumu yeyote katika mochwari hiyo ambaye ametiwa mbaroni wala kuchukuliwa hatua yoyote

Msemaji huyo wa polisi alizidi kusema kwamab kitoto hicho kilifariki kutokana na kukosa hewa safi ya kupumua na kifo chake kilikuwa cha utata miongoni mwa vifo vingi vya vitoto vichanga ambavyo vimeripotiwa katika taasisi hiyo ya afya – kuishuritisha dola kuchukua jukumu la kuanzisha uchunguzi kubaini kifo.