Pasta aliyealikwa shuleni kuwaombea wanafunzi atoroka na binti wa kidato cha 4

Inaarifiwa mchungaji huyo pindi baada ya kufika katika shule hiyo, aliondoka na mwanafunzi wa kike na kuabiri bodaboda naye na inakisiwa walivuka kwenda kaunti jirani ya narok.

Muhtasari

• Mwanafunzi huyo alikuwa miongoni mwa watahiniwa wa mitihani ya kitaifa KCSE mwaka huu.

Mchu8ngaji aingia mitini na mwanafunzi
Mchu8ngaji aingia mitini na mwanafunzi
Image: BBC NEWS

Mchungaji mmoja katika kaunti ya Bomet yuko mafichoni baada ya kudaiwa kutoroka na mwanafunzi wa kike mtahiniwa wa kidato cha nne baada ya kualikwa katika shule moja kwa ajili ya maombi kwa watanihiwa wa mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopeperushwa na Citizen, ibada ya kuwaombea watahiniwa wa KCSE mwaka huu katika shule ya upili ya Ngererit yalisitishwa baada ya kubainika kwamba mchungaji huyo alichimba mitini na mwanafunzi mmoja wa kike.

Katika ripoti ya polisi iliyowasilishwa katika kituo cha polisi cha Konoin, inadaiwa mshukiwa alionekana mara ya mwisho akipanda bodaboda na mwanafunzi huyo katika kituo cha biashara cha Mogogosiek kabla ya kutoweka kwenye barabara ya vumbi ya matope bila kujulikana Zaidi, ripoti hiyo ilisema.

Kulingana na mkurugenzi wa elimu kaunti ya Bomet Leonard Ngugi, idara yake ilimtahadharisha OCS wa eneo hilo kuhusu kisa hicho. Wawili hao wanasemekana kuvuka hadi kaunti jirani ya Narok.

"Tunatumai kuwa polisi wanafanya juhudi za kuwakamata popote walipo ili wazazi wakabidhiwe mtoto wao ili aendelee na masomo yake. Inasikitisha kwamba mwanafunzi huyo sasa anapaswa kusahihisha mitihani yake ya kitaifa," Ngugi alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Wazazi wa Kaunti ya Bomet (PTA) Stephen Kosgei alizitaka shule kuwa waangalifu kuhusu wageni kuingiliana na wanafunzi.

Ifahamike kwamba serikali ilipiga marufuku hafla za maombi kwa ajili ya watahiniwa wa mitihani ya kitaifa shuleni katika muhula wa tatu.

Shule nyingi zimelazimika kufanya hafla hiyo mwishoni wa muhula wa pili na zingine mwanzoni mwa muhula wa tatu ili kuendana na agizo la serikali kutotana maombi kufanyika wakati mitihani imekaribia kufanyika.