“Kuna kazi niliahidi kufanya?” Karen Nyamu ajibu kuhusu kuibuka seneta aliyechangia kidogo seneti

Seneta Karen Nyamu alizungumza mara 17 katika seneti pekee tangu kujiunga na bunge hilo.

Muhtasari

•Nyamu amejibu kwa kejeli kuhusu kuorodheshwa miongoni mwa maseneta vijana walio na mchango mdogo zaidi katika seneti.

•Karen Nyamu na maseneta wenzake wa kuteuliwa Hezena Lamaletian na Chimera Mwinzago waliorodheshwa kama maseneta vijana waliochangia kidogo zaidi katika seneti.

Karen Nyamu.
Karen Nyamu.
Image: Facebook

Wakili Karen Nyamu amejibu kwa kejeli kuhusu kuorodheshwa miongoni mwa maseneta vijana walio na mchango mdogo zaidi katika seneti.

Siku ya Alhamisi, mwanamitandao mmoja alimshauri seneta huyo kufanya kazi kwa bidii huku akimkumbusha kuwa alishikilia nafasi mbaya katika orodha iliyotolewa hivi majuzi ya michango ya hoja ya maseneta katika seneti.

"Ebu fanya kazi yako, uliona kadi yako ya alama? Kazi ni kuwasumbua akina mama na watoto na hufanyi kazi," mtumiaji wa mtandao wa Instagram alitoa maoni yake chini ya moja ya posti za seneta Karen Nyamu.

Katika majibu yake, seneta huyo wa kuteuliwa alibainisha kwa utani kwamba hakuwahi kuahidi kufanya kazi yoyote.

"Kuna kazi niliahidi kufanya?" Karen alijibu na kuambatanisha jibu lake kwa emoji za kucheka.

Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Karen Nyamu na maseneta wenzake wa kuteuliwa Hezena Lamaletian na Chimera Mwinzago waliorodheshwa kama maseneta vijana waliochangia kidogo zaidi katika seneti katika ripoti iliyotolewa hivi majuzi.

Ripoti ya Mzalendo Trust, ambayo ni ripoti ya matokeo ya kwanza ya Bunge la 13 ilisema kuwa maseneta hao watatu walizungumza chini ya mara 27.

Mwinzago na Nyamu ambao ni wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) walizungumza mara 23 na 17 mtawalia.

Huku Hezena ambaye ameteuliwa na chama cha Orange Democratic Movement (ODM) akizungumza mara 21 pekee.

Ripoti ya matokeo ya Bunge ya 2023 inajumuisha kipindi cha kati ya Septemba 29, 2022, hadi Juni 30, 2023.

Seneta Nyamu amekuwa akigonga vichwa vya habari kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita kufuatia uhusiano wake na msanii wa Mugithi, Samidoh.

Mapema mwaka huu, alifika mbele ya kamati ya nidhamu ya UDA kujibu tuhuma zilizomkabili.

Mashtaka dhidi ya seneta huyo yanahusu mwenendo wake 'wa aibu' mnamo Desemba 16, 2022 ambapo alizua drama katika tamasha la Samidoh jijini Dubai na kusababisha mzozo na mkewe Edday Nderitu.