YouTube kufuta video za mahubiri na maombi ya uponyaji wa UKIMWI na saratani

Video hizo pia ni pamoja na zile zinazowashauri wagonjwa hao wa saratani na UKIMWI kutumia kitunguu saumu au kula vyakula vyenye vitamini C badala ya kupata matibabu kwa njia sahihi za radioherapy na ARV.

Muhtasari

• Tangazo hili linakuja wakati nchini Kenya kumekuwa na mjadala mkali kuhusu baadhi ya mahubiri yenye ukakasi kutoka kwa wahubiri.

• YouTube ilisema wachungaji wanawapotosha watu kuwa maombi yanaponya, jambo ambalo si kweli na linawahadaa wagonjwa kutotafuta matibabu sahihi.

YouTube yalegeza masharti ya wakuza maudhui kujiung mpango wa malipo
YouTube yalegeza masharti ya wakuza maudhui kujiung mpango wa malipo
Image: Facebook

Gazeti la Taifa Leo linaripoti kwamba mamlaka ya jukwaa la video la YouTube inatathmini kufuta video zote ambazo ni za mahubiri na maombi ya wachungaji wanaojidai kwamba wanaponya magonjwa sugu kama saratani na Ukimwi kupitia maombi tu pasi na dawa yoyote.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mtandao huo wa kijamii ulisema kuwa, “Kwa siku na wiki zijazo, tutaondoa video zote zinazoeleza kuhusu matibabu ya kansa ambazo si za kweli na zinapotosha wagonjwa kwa kuwafanya wasitafute matibabu.”

Video hizo pia ni pamoja na zile zinazowashauri wagonjwa hao wa kansa kutumia kitunguu saumu au kula vyakula vyenye vitamini C badala ya kupata matibabu kwa njia ya mtambo wa kisasa unaotoa miale ya X-Ray kuua seli zinazosambaza saratani (radiotherapy), Taifa Leo walieleza.

“Pia tutaweka kizuizi cha umri au kuwa na paneli ya watu watakaoangazia maudhui ya video ili kuongezea ujumbe uliopo,” gazeti hilo lilinukuu YouTube.

Tangazo hili linakuja wakati nchini Kenya kumekuwa na mjadala mkali kuhusu baadhi ya mahubiri yenye ukakasi kutoka kwa wahubiri.

Wengine wamefikia hatua ya kudai kwamba wana uwezo na nguvu za kufufua maiti, wengine hata kuponya kizazi cha tasa na kumfanya kupata mtoto, wengine kuwaponya viwete, vipofu, vichaa na mahubiri mengine ya kutiliwa shaka.

Katika miezi michache iliyopita, mhubiri anayejiita nabii wa Mungu David Owuor alidai kwamba aliponya watu wengi katika ziara yake ya maombi ya uponyaji kwenye eneo pana la Bonde la Ufa.

Kwa mujibu wa kamati ya bunge la seneti iliyokuwa inachunguza mauaji ya halaiki katika msitu wa Shakahola, ilielezwa kwamba watu kadhaa walijitokeza na kudai kwamba walipata uponyaji kutokana na programu za mchungaji huyo tata.

Dkt Toromo Kochei, mratibu wa eneo la Bonde la Ufa wa Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Ukimwi (NASCOP) aliambia kamati hiyo kuwa chini ya mamlaka ya NASCOP, alifanya historia ya kina ya wagonjwa waliodai kuponywa na kugundua kuwa walikuwa wamepona kabisa.

Aliipa kamati hiyo angalau majina matatu ya wagonjwa wa ukimwi wanaodaiwa kuponywa ugonjwa huo kwa njia ya imani, akisema kuwa taarifa za wagonjwa kuponywa kwa njia ya miujiza si za kushabikia.

Fauka ya hayo, wiki iliyopita setikali ilitoa orodha ya makanisa kadhaa ambayo leseni zao za kuhudumu zimefutiliwa mbali yakiwemo ni pamoja na yale ya mchungaji tata Paul Mackenzi bila kumsaza Ezekiel Odero.