MP wa UDA West Pokot ajuta kuunga Ruto mkono 'Anaweza fanya hata nisiende mbinguni'

"Mimi ni mwanachama wa UDA, najuta kwanini nilimchagua huyu ambaye wakati mwingine anaweza kunifanya nisiwe mbinguni, naomba msamaha kwa Mungu,” alilalamika.

Muhtasari

• Moroto aliomba msamaha kwa uamuzi wake wa kuunga mkono utawala wa sasa.

• Hisia za Moroto zilikuja baada ya watu sita kuuawa katika shambulizi la ujambazi katika eneo la Sarmach katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Samuel Moroto
Samuel Moroto
Image: X

Samwel Moroto, mbunge wa Kapenguria kaunti ya West Pokot ameonesha kukerwa kwake na serikali iliyopo uongozini ya UDA akisema kwamba anajuta pakubwa kumuunga rais Ruto mkono katika uchaguzi wa mwaka jana.

Mbunge huyo ambaye aliingia bungeni kwa tikiti cha chama tawala cha UDA alisema kwamba serikali ya Kenya Kwanza baadhi ya viongozi wake ndio wanaochochea vita na wizi wa mifugo unaoendelea katika kaunti ya West Pokot.

Moroto kwa ukali na kujuta alisema kwamba huenda hata akakosa nafasi ya kuingia mbinguni kutokana na kumuunga Ruto na serikali ya Kenya Kwanza mkono.

Moroto aliomba msamaha kwa uamuzi wake wa kuunga mkono utawala wa sasa.

“Sehemu hii ya chini ndiyo serikali inayochochea hii si serikali nyingine, ni hii, hata mimi ni mwanachama wa UDA, najuta kwanini nilimchagua huyu ambaye wakati mwingine anaweza kunifanya nisiwe mbinguni, naomba msamaha kwa Mungu,” alilalamika.

Hisia za Moroto zilikuja baada ya watu sita kuuawa katika shambulizi la ujambazi katika eneo la Sarmach katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Watu watatu kati ya waliofariki ni watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliokuwa wamevamia kijiji hicho, wengine wawili walikutwa na majibizano ya moto kati ya majambazi hao na kikosi cha ulinzi kinachofanya operesheni ya ulinzi mkoani humo. Mwingine aliyejeruhiwa alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Kapenguria.

Majambazi wamekuwa wakiendeleza vita katika baadhi ya kaunti za kaskazini mwa Bonde la Ufa na kuwaua watu licha ya ziara za mara kwa mara za waziri wa usalama wa ndani profesa Kithure Kindiki.