"Mwanaume mwenye sura nzuri zaidi Afrika!" Gavana Kawira Mwangaza ajigamba kuhusu mumewe Murega Baichu

Gavana Kawira Mwangaza pia hakumaliza mahubiri yake bila kujigamba kuwa mke kamili.

Muhtasari

•Gavana huyo aliyezingirwa na utata mwingi alimtawaza mumewe kwa vyeo vikubwa vikubwa katika harakati za kumsherehekea.

•Gavana Kawira Mwangaza alijigamba kuhusu kuwa na mwanamume mwenye sura nzuri zaidi.

wakati wa uzinduzi wa baraza la mawaziri la kaunti ya Meru mnamo Septemba 30, 2022.
Gavana wa Meru Kawira Mwangaza na mumewe Murega Baichu wakati wa uzinduzi wa baraza la mawaziri la kaunti ya Meru mnamo Septemba 30, 2022.
Image: FACEBOOK// HON KAWIRA MWANGAZA

Gavana wa Meru, Kawira Mwangaza amemmiminia sifa  hadharani mume wake Robert Murega Baichu wiki chache tu baada ya kunusurika kuondolewa madarakani.

Alipokuwa akitoa mahubiri katika ibada ya hivi majuzi katika Kanisa la Jesus House of Praise, mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata mwingi alimtawaza mumewe kwa vyeo vikubwa vikubwa katika harakati za kumsherehekea.

"Anaitwa mume wa gavana mwenyewe, ndiyo, mume wa gavana mwenyewe," Kawira Mwangaza aliwaambia washarika waliokuwa wamehudhuria ibada hiyo kwa ujasiri.

Aliendelea kujigamba kuhusu kuwa na mwanamume mwenye sura nzuri zaidi na akazungumza kuhusu jukumu kubwa la mwanamuziki huyo katika taaluma yake ya kisiasa.

“Yeye ndiye kamanda wa Shirika la Ndege la Ameru, mwenye sura nzuri zaidi barani Afrika na baadhi ya sehemu za Ulaya. Mshauri wa kisiasa wa gavana wa Kaunti ya Meru, na John Mbatizaji wa leo kwa gavana,” akasema.

Gavana Kawira Mwangaza pia hakumaliza mahubiri yake bila kujigamba kuwa mke kamili.

“Ndiye mwanamume pekee aliyebarikiwa kuwa mke anayestahili. Mwanaume pekee mwenye wife material. Makofi kwake jamani,” alisema.

Hisia hizi zinakuja wiki chache tu baada ya gavana huyo wa muhula wa kwanza kuokolewa na seneti baada ya MCAs wa Kaunti ya Meru kumng’oa madarakani kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kuhusika kwa mume wake Murega Baichu katika masuala ya kaunti.

Mapema mwezi uliopita, jumla ya maseneta 47 walikosa kushikilia mashtaka yoyote kati ya saba yaliyotajwa dhidi yake na Bunge la Kaunti ya Meru ambalo lilipiga kura kwa kauli moja kumfukuza afisini.

Gavana huyo alikuwa ameshtakiwa kwa matumizi mabaya ya rasilimali za kaunti, upendeleo wa kindugu na mila potofu, uonevu na kuwatusi viongozi wengine, kupora mamlaka yake ya kisheria, kudharau mahakama, kutaja barabara ya umma kinyume cha sheria kwa jina la mumewe na kudharau Bunge la Kaunti ya Meru.

Baada ya kusikilizwa kwa siku mbili kwa kesi ya kuondolewa madarakani dhidi yake, Maseneta 47 walipiga kura muhimu , wakipiga kura kwa kila moja ya makosa saba yaliyoelekezwa dhidi ya Gavana Mwangaza.