Mapasta kaunti ya Kiambu wamuomba Ruto kupunguza kasi za tozo na ushuru 2024

Mwaka wa 2023 ndio mwaka ambao bunge lilipitisha mswada wa fedha ambao umetajwa na wengi haswa kutoka mrengo wa upinzani kuwa unaowakandamiza wananchi.

Muhtasari

• "Lakini nataka kuomba serikali yetu, kwa sababu tumeruka mwaka mwingine, wajaribu kuangalia mambo ya ushuru" 

Mapasta Kiambu
Mapasta Kiambu
Image: Facebook//screenshot

Wachungaji wa makanisa mbalimbali katika kaunti pana ya Kiambu wametoa wito kwa rais Ruto kupunguza kasi ya tozo na ushuru kwa Wakenya katika mwaka huu mpya wa 2024, wakidai kwamba mwaka wa 2023 umekuwa mgumu kwa Wakenya wengi kutokana na nyongeza ya tozo mbalimbali.

Wachungaji hao walikuwa wanazungumza katika mkutano wa pamoja siku ya mwisho ya mwaka 2023 ambapo walimtaka kiongozi wa nchi kuzingatia kurahisisha maisha kwa wapiga kura kwa kupunguza au kuondoa baadhi ya ushuru ambao umekuwa mzigo mzito kwao.

“Nataka kushukuru mwenyezi Mungu kwa kutufikisha mwisho wa mwaka huu, huu mwaka umepita umekuwa mgumu, watu hawana kitu kwa mfuko na hata sikukuu hii watu wamekula kwa njia ya kung’ang’ana. Lakini nataka kuomba serikali yetu, kwa sababu tumeruka mwaka mwingine, wajaribu kuangalia mambo ya ushuru ule umefinyilia mwananchi, na wakiangalia mambo yatakwua sawa kwao,” mmoja alisema.

“Tuko na matarajio mazuri kwamba serikali yetu itatengeneza uchumi na mambo yatakuwa sawa ili kila mkenya akaweze kutosheka akiwa nchini humu kwa sababu tunajivunia kuwa Wakenya,” mwingine aliongeza.

“Mwaka wa 2023 umekuwa mgumu haswa kwa wale wako chini, imekuwa vigumu kwao kupata chakula, watoto kusoma imekuwa shida. Kama wakati huu watoto wanapotarajia kurudi shule, tumeona ugumu kwa sababu wengi hawajui watarudisha watoto shule aje, lakini tuko na Imani ya kwamba serikali ikiweka mambo jinsi inavyotakikana, kutakuwa na ubadilishanaji wa mambo,” mwingine wa kike aliongeza.

Mwaka wa 2023 ndio mwaka ambao bunge lilipitisha mswada wa fedha ambao umetajwa na wengi haswa kutoka mrengo wa upinzani kuwa unaowakandamiza wananchi wa kawaida wenye kipato cha chini kiuchumi.