Jamaa ashtaki hoteli baada ya 'scorpion' kumuuma kwenye sehemu za siri akiwa amelala

Mlalamishi amedai kwamba aliamshwa na maumivu makali kwenye sehemu za siri kabla ya kuona nge amekwama kwenye chupi yake.

Muhtasari

•Michael Farchi alidai kuwa mdudu aina ya nge alimuuma kwenye korodani wakati akiwa amelala kwenye moja ya vyumba vya hoteli.

•Alidai aliumwa takriban mara tatu na kiumbe huyo ambaye hatimaye alimkuta amekwama kwenye chupi yake.

Nge
Image: HISANI

Mwanaume mmoja kutoka Marekani ambaye alikuwa akifurahia likizo yake katika hoteli moja ya kifahari jijini Las Vegas, katika jimbo la Nevada, akidai kuwa mdudu aina ya nge alimuuma kwenye korodani wakati akiwa amelala kwenye moja ya vyumba vya hoteli hiyo.

Michael Farchi ambaye anatokea California na familia yake walikuwa wakikaa kwenye mnara wa Palazo mnamo Desemba 26, 2023 alipodaiwa kuamshwa na maumivu makali kwenye sehemu za siri.

Aliiambia Eyewitness News kwamba aliachwa na maumivu makali baada ya nge huyo kumng'ata na kusisitiza kuwa bado anakabiliwa na matatizo ya kiafya miezi kadhaa baada ya tukio hilo.

“Niliamka na maumivu makali katika eneo langu la siri,” alidai.

Aliongeza, "Sikujua ni nini. Nilinyoosha mkono wangu kuona kinachotokea chini ya blanketi na nikapata maumivu mengine makali."

Alidai aliumwa takriban mara tatu au nne na kiumbe huyo mdogo mwenye sumu, ambaye hatimaye alimkuta bado amekwama kwenye chupi yake. Baadaye alitibiwa katika hospitali ya eneo hilo na kuandikisha ripoti kwa wafanyikazi wa hoteli hiyo.

Aina halisi ya nge ambaye inadaiwa kumng'ata mwanaume huyo, na ukali wa sumu yake, haijulikani wazi. Picha zilizoshirikiwa na mwathiriwa na wakili wake hata hivyo zinaonyesha mdudu huyo mdogo anaonekana kuwa na urefu wa inchi moja.

Bw Farchi amedai kuwa licha ya tukio hilo, bado aliulizwa malipo ya chumba hicho. Sasa anashtaki hoteli hiyo ya mapumziko kwa kiasi ambacho hakijabainishwa.

"Hakuna mtu anayekaa Vegas anayehitaji kuonyeshwa nge wabaya wakati wamelala, achilia sehemu zao za siri, korodani zao," wakili Brian Virag alisema.

Ilipowasiliana na kituo cha televisheni cha Las Vegas, hoteli hiyo ilisema kwamba mikakati iliyowekwa ilifuatwa katika tukio hilo.

"Mapumziko hayo yana itifaki za matukio yote na tunaweza kuthibitisha yalifuatwa katika tukio hili," wasimamizi walisema.

Ulimwengu mzima sasa unasubiri kuona ikiwa mlalamishi atawasilisha kesi kali dhidi ya hoteli hiyo na atalipwa kiasi gani iwapo atafaulu.