Rais Ruto amzomea Mbunge Peter Salasya kwa kutochana nywele zake

Salasya aliahidi kutengeneza nywele zake ikiwa rais atamamuru afanye hivyo.

Muhtasari

•Rais aliwafanya viongozi wengine kuangua kicheko kikubwa alipomuuliza mbunge huyo wa muhula wa kwanza sababu iliyomfanya asichane nywele.

•Ruto aliendelea na mazungumzo akimuuliza kwa nini hakuwa amechana nywele zake.

akisalimiana na Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya alipowasili Kakamega kufungua Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji la Kaunti mnamo Machi 20, 2024.
Rais William Ruto akisalimiana na Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya alipowasili Kakamega kufungua Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji la Kaunti mnamo Machi 20, 2024.
Image: INSTAGRAM// PETER SALASYA

Video inayoonyesha rais William Ruto akimfanyia mzaha mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya kuhusu nywele zake zilizochanika imesambaa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Katika video hiyo iliyorekodiwa Kakamega siku ya Jumatano, rais aliwafanya viongozi wengine kuangua kicheko kikubwa alipomuuliza mbunge huyo wa muhula wa kwanza sababu iliyomfanya asichane nywele zake.

Rais alikuwa akiwasalimu viongozi  wengine alipowasili Kakamega kufungua Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji la Kaunti ya Kakamega wakati  alipokutana na Salasya.

Wabunge wa Bunge la Kitaifa na Seneti walikuwa wamejipanga kumkaribisha Rais katika kaunti hiyo ya Maghabribi mwa Kenya.

Huku akiwasalimia kwa mkono viongozi hao, aliwaita kwa majina akiuliza jinsi maeneo ambayo wanawakilisha yanaendelea.

Hatimaye zamu ya ,bunge Peter Salasya ilifika, na alionekana kuwa na shauku ya kumsalimia kiongozi huyo wa taifa.

Mbunge huyo wa Mumias Mashariki alimpa rais mikono yake kwa nguvu huku akiegemeza macho yake moja kwa moja kwa kamera.

Rais alimuuliza anaendeleaje na akamjibu anaendelea vizuri huku akiwa na tabasamu kubwa.

Jibu lake likapelekea viongozi wengine kuangua vicheko.

Ruto aliendelea na mazungumzo akimuuliza kwa nini hakuwa amechana nywele zake.

“Mbona haujachanua nywele,” Rais aliuliza.

Mbunge akajibu kwa mbwembwe nyingi alijibu "Ukisema nitachanua".

Jibu lake lilipelekea Rais na wengine waliokuwepo kuangua kicheko.

Mbunge huyo wa muhula wa kwanza anajulikana kwa staili yake ya nywele ndefu kidogo ambayo aghalabu huwa hachani.

Rais Ruto alifungua rasmi Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji la Kaunti ya Kakamega mnamo siku ya Jumatano.