Sudan Kusini: Jamaa atumia miale ya jua kukaanga mayai hali ya joto kali ikizidi kuwa mbaya (video)

Wiki mbili zilizopita, serikali ya Sudan Kusini ilifunga shule kutokana na joto kali kote nchini.

Muhtasari

• Sudan Kusini katika miaka ya hivi karibuni imekumbwa na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa, huku joto kali, mafuriko na ukame ukiripotiwa katika misimu tofauti.

• Wakati wa wimbi la joto wiki mbili zilizopita, nchi ilisajili viwango vya joto hadi nyuzi joto 45 (113 Fahrenheit).

Sudan Kusini joto lazidi kuwa kali
Sudan Kusini joto lazidi kuwa kali
Image: screengrab

Hali ya joto kali kutokana na jua kali nchini Sudan Kusini inazidi kuwa mbaya Zaidi kama kile kinachoonekana mitandaoni ni cha kuaminiwa.

Katika video moja ambayo imewavutia wengi, kijana mwenye umri wa makamo alionekana kuingia jikoni na kutoka nje akiwa na sufuria na yai tayari kwa kulikaanga, kasoro moto tu.

Cha kushangaza ni kwamba kijana huyo alipasua yai na kuliweka kwenye sufuria kabla ya kuanika kwenye jua akitumai kutumia miale ya jua kali kuliivisha yai lake.

Yai lile lilionekana likichemka kutokana na miale na jua kali, hali ambayo imekuwa ikikumba wakaazi wengi wa taifa hilo changa kabisa barani Afrika kwa Zaidi ya wiki mbili sasa.

Wiki mbili zilizopita, serikali ya Sudan Kusini ilifunga shule kutokana na joto kali kote nchini.

Wizara ya afya na elimu ilisema hali ya joto inatarajiwa kushuka kwa kasi huku msimu wa mvua ukitarajiwa kuanza katika siku zijazo.

Sudan Kusini katika miaka ya hivi karibuni imekumbwa na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa, huku joto kali, mafuriko na ukame ukiripotiwa katika misimu tofauti.

Wakati wa wimbi la joto wiki mbili zilizopita, nchi ilisajili viwango vya joto hadi nyuzi joto 45 (113 Fahrenheit).

Walimu walihimizwa kupunguza shughuli za uwanja wa michezo hadi asubuhi na mapema au ndani ya nyumba, kuingiza hewa ndani ya vyumba vya madarasa, kutoa maji wakati wa shule na kufuatilia watoto kwa dalili za uchovu wa joto na kiharusi.