Gachagua hakufadhili kongamano la Limuru III- Kioni aweka wazi

Alisisitiza kuwa hii ni mara ya kwanza kwa tukio hilo kuendeshwa na wananchi.

Muhtasari
  • Akizungumza Jumatano, Kioni alisema kongamano hilo lilitokana na juhudi za pamoja na uungwaji mkono wa wananchi kutoka eneo la Mlima Kenya.
Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee Jeremiah Kioni
Image: Jeremiah Kioni /TWITTER

Katibu mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni amekanusha ripoti kuwa kongamano la Limuru III lilifadhiliwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Akizungumza Jumatano, Kioni alisema kongamano hilo lilitokana na juhudi za pamoja na uungwaji mkono wa wananchi kutoka eneo la Mlima Kenya.

Alisisitiza kuwa hii ni mara ya kwanza kwa tukio hilo kuendeshwa na wananchi.

Kioni alisema kuwa watu hao walikuwa na maswala ambayo walitaka kushughulikia na ndivyo ilifanyika.

"Yeye (Gachagua) hakufanya hivyo. Haikufadhiliwa na mtu yeyote. Ilikuwa Limuru III iliyojifadhili yenyewe, tofauti na siku za nyuma.

“Watu walitumia rasilimali zao na walikuja kwa wingi na kutaka kuongea na walisema masuala yao,” alisema kwenye KTN News.

Baadhi ya viongozi kutoka eneo hilo walidai kuwa "mtu fulani" alikuwa akifadhili hafla hiyo.

Mkutano wa Limuru III ulifanyika Mei 17, 2024. Ulizaa muungano mpya wa Mlima Kenya uliopewa jina la Haki Coalition.

Muungano huo unaundwa na zaidi ya vyama 26 vya kisiasa kutoka eneo la Mlima Kenya.

Waandalizi wa mkutano wa Limuru III wa kijamii na kiuchumi na kisiasa walikuwa wamesema kuwa Gachagua na rais wa zamani Uhuru Kenyatta wanakaribishwa kuhudhuria kongamano hilo.

Kabla ya kongamano hilo, Gachagua alikuwa ametoa wito kwa Kioni na Karua kushauriana naye kuhusu masuala yanayohusiana na Mlima Kenya.