Kazi yangu sio kukaa ofisini tu! Murkomen amjibu Malala

Mnamo Jumatano, katibu mkuu wa UDA Cleophas Malala aliwaita Murkomen na mwenzake wa Utumishi wa Umma Moses Kuria kwa madai ya kujihusisha na siasa.

Muhtasari
  • Murkomen alizungumza Ijumaa akiwa Kijabe katika ziara ya kukagua sehemu zilizoharibika za njia ya reli ya kupima mita.
  • Murkomen alisisitiza uelewa wake wa jukumu lake akidai kwamba hahitaji mawaidha yoyote au maagizo ya jinsi ya kuitekeleza.
Waziri Kipchumba Murkomen
Image: MAKTABA

Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen ametamka kwa uthabiti kwamba hataruhusu mtu yeyote kuamuru jinsi anafaa kutekeleza majukumu yake.

Murkomen alisisitiza uelewa wake wa jukumu lake akidai kwamba hahitaji mawaidha yoyote au maagizo ya jinsi ya kuitekeleza.

"Kuna wengine wananiambia ati nikae huko kwa ofisi tu, ati nikae kwa kiti niitwe waziri na nisipatikane nikitembea na wabunge," alisema.

Murkomen alizungumza Ijumaa akiwa Kijabe katika ziara ya kukagua sehemu zilizoharibika za njia ya reli ya kupima mita.

Mnamo Jumatano, katibu mkuu wa UDA Cleophas Malala aliwaita Murkomen na mwenzake wa Utumishi wa Umma Moses Kuria kwa madai ya kujihusisha na siasa.

“Imefahamika kuwa baadhi ya Mawaziri wamekuwa wakijihusisha na shughuli za kisiasa kinyume na sheria inayowataka kubaki kisiasa,” alisema.

Malala aliendelea kusema kwamba iwapo Mawaziri watahisi haja ya kujihusisha na siasa kikamilifu, wanapaswa kujiuzulu kutoka ofisi za umma wanazoshikilia.

"Vile vile, Kipchumba Murkomen,waziri wa Barabara na Uchukuzi, mkazo wako unapaswa kuwa katika kushughulikia maswala muhimu katika wizara yako, haswa ukarabati wa barabara zilizoharibiwa na mafuriko ya hivi majuzi. Watumikie Wakenya au uondoke kwenye nafasi yako na urudi kwenye siasa. ,” Malala aliongeza.

Murkomen alisema hatalegea katika ziara zake za mara kwa mara katika kaunti kukutana na wananchi na kusikiliza maswala yao.