Vitunguu, nyanya, sukumawiki na viazi zapanda bei maradufu kutokana na mfumko wa bei

Bei na kodi ya juu ya nyumba, umeme, gesi, na aina tofauti za mafuta pia zilichangia mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali humu nchini katika kipindi cha mwezi uliopita.

Bidhaa za nyanya na vitunguu sokoni
Bidhaa za nyanya na vitunguu sokoni
Image: BBC

Bei za bidhaa za vyakula mbalimbali kutoka shambani ziliripotiwa kupanda maradufu kati ya mwezi Aprili na Mei.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya KNBS iliyochapishwa katika gazeti la Taifa Leo, bei za bidhaa kama vile vitunguu, sukumawiki na viazi ilishuhudiwa kuongezeka kwa hadi asilimia 5.1 katika mwezi wa Mei kutoka asilimia 5.0 mwezi wa Aprili.

Ripoti hiyo inabaini kwamba bei na kodi ya juu ya nyumba, umeme, gesi, na aina tofauti za mafuta pia zilichangia mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali humu nchini katika kipindi cha mwezi uliopita.

Hii ilifanya bei ya kitunguu kuuzwa kwa Sh188.37 kwa kilo kutoka Sh177.02 huku kilo ya Spinachi ikiuzwa kwa Sh88.37 kutoka Sh74.78 mwezi wa Aprili.

Katika kipindi hicho, bei za sukumawiki ziliongezeka kwa asilimia 18.2, nyanya (asilimia 15) na viazi (asilimia 6.2), Taifa Leo waliidadavua ripoti hiyo.

Hata hivyo, bei za unga wa mahindi yaliyosagwa, unga wa mahindi ulioimarishwa, unga wa mahindi na unga mweupe wa ngano ilipungua kwa asilimia 3.2, 2.3, 1.6 na 1.3 mtawalia.

“Bei za nyumba, maji, umeme, gesi na aina zote za mafuta ziliongezeka kwa asilimia 1.2 kati ya Aprili 2024 na Mei 2024 kutokana na kupanda kwa bei ya kWh 200 na kWh 50 za umeme kwa asilimia 6.9 na asilimia 5.5 mtawalia,” takwimu kutoka KNBS zinaonyesha kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Gharama ya usafiri iliongezeka kwa asilimia 0.2 baada ya bei ya petroli na dizeli kushuka kwa asilimia 0.5 na asilimia 0.7 mtawalia.