Siaya: Taharuki maiti ya mtoto wa siku 1 ikiibwa kutoka kaburini siku 10 baada ya maziko

Familia hiyo ilisema kwamba kilichowatia wasiwasi na hofu zaidi ni kwamba mwili wa mtoto huyo ulichukuliwa uchi, kwani walipata nguo zote walizomzika nazo zikiwa pembezoni mwa kaburi lake.

Muhtasari

• Ripoti hiyo ilibaini kwamba mtoto huyo alifariki hata kabla ya kupatiwa jina na hivyo rekodi za hospitalini zilimtambua tu kama kitoto kichanga.

• Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi na uchunguzi umeanzishwa.

Jeneza tupu.
Jeneza tupu.
Image: Maktaba

Hali ya taharuki na simanzi imetanda katka kijiji cha Kamhinda kaunti ya Siaya baada ya wanafamilia kuamka na kupata kaburi la mtoto wao likiwa wazi bila chochote ndani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kuvunja moyo iliyochapishwa kwenye jarida la Nation, walimzika mpendwa wao ambaye ni mtoto aliyezaliwa na kufa saa chache baadae.

Hata hivyo, siku 10 baadae, walipigwa na butwaa kurauka asubuhi na kupatana na taswira isiyo nzuri kwani kaburi la mtoto huyo aliyedumu duniani kwa saa 3 tu lilikuwa wazi na maiti yake kutoweka.

“Baada ya mtoto kufa hospitalini saa 3 baada ya kuzaliwa, tulichukua mwili na kuuzika katika boma langu, Mei 28. Lakini Ijumaa iliyopita tulirauka na kupata kaburi li wazi bila mwili,” babake mtoto huyo aliyetambuliwa na jarida hilo kwa jina Joseph Origi alieleza kwa majonzi.

Baba huyo akiwa kwenye uchungu, alisema kwamba tukio hilo lilikuja kama msumari moto kwenye kidonda kwani familia bado ilikuwa haijapona kutokana na kufiwa kwa mtoto wao kabla ya tukio lingine la mwili kutoweka kutoka kaburini kujiri.

Alisema kwamba tukio hilo limeiacha familia katika hali ya mshtuko mkubwa, ikizingatiwa kwamba walibaini mwanao huenda alichukuliwa uchi kwani nguo zote walizomzika nazo walizipata pembezoni mwa kaburi lake.

“Ni jambo la kushangaza kwamba kila kitu ambacho tulimvalisha mtoto tulikipata pembezoni mwa kaburi, zikiwemo soksi zake,” aliongeza kwa uchungu.

Ripoti hiyo ilibaini kwamba mtoto huyo alifariki hata kabla ya kupatiwa jina na hivyo rekodi za hospitalini zilimtambua tu kama kitoto kichanga.

Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi na uchunguzi umeanzishwa.