"Anapenda kujifunga bao" Mwangi amkosoa Raila kwa kumtembelea Ezekiel baada ya kuachiliwa

Mwanaharakati Boniface Mwangi alitaja hatua ya Raila kama kujifunga bao.

Muhtasari

•Raila alimtembelea Mchungaji Ezekiel Odero Jumamosi katika kanisa lake la New Life Prayer Centre and Church iliyo kaunti ya Kilifi.

•Mwangi alimshtumu Raila Odinga kwa kutojifunza kutokana na makosa yake ya siku za nyuma.

amemkosoa kinara wa ODM Raila Odinga kwa kumtembelea mchungaji Ezekiel Odero
Boniface Mwangi amemkosoa kinara wa ODM Raila Odinga kwa kumtembelea mchungaji Ezekiel Odero
Image: HISANI

Mwanaharakati maarufu Boniface Mwangi amemkosoa kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja- One Kenya, Raila Odinga kufuatia hatua yake kumtembelea mchungaji Ezekiel Odero siku chache baada ya kuachiliwa kwa dhamana..

Siku ya Jumamosi, Raila alimtembelea mtumishi huyo wa Mungu anayechunguzwa kwa madai ya kuhusishwa na ibada ya Shakahola katika kanisa lake la New Life Prayer Centre and Church iliyo kaunti ya Kilifi. Baadaye waliandamana hadi kwenye jumba la kifahari la mchungaji huyo ambapo walifanya mazungumzo.

Akizungumzia ziara hiyo kwenye akaunti yake ya Twitter, mwanaharakati Mwangi alitaja hatua ya Raila kama kujifunga bao.

"Raila Odinga anapenda kujifunga bao mwenyewe," alisema siku ya Jumamosi jioni.

Mwandani huyo wa aliyekuwa mgombea mwenza wa Azimio-One Kenya, Bi Martha Karua aliendelea kumshtumu Raila Odinga kwa kutojifunza kutokana na makosa yake ya siku za nyuma.

"Maisha ni ya kikatili kwa wale ambao hawajifunzi kutokana na makosa yao ya zamani," Mwangi alisema.

Mwangi ni miongoni mwa wanaharakati waliounga mkono azma ya kinara huyo wa ODM kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana na ameendelea kutetea muungano wa Azimio huku akikosoa utawala wa Kenya Kwanza.

Raila alichukua hatua ya kumtembelea Ezekiel Jumamosi baada ya kuhudhuria hafla ya maziko katika eneo la Chonyi, Kaunti ya Kilifi. Walikuwepo pia wakili Cliff Ombeta na Gavana wa Kilifi Gideon Mung'aro katika ziara hiyo.

Raila ndiye kiongozi wa kwanza wa kitaifa kukutana na Mchungaji Ezekiel tangu aachiliwe kutoka mikononi mwa polisi siku ya Alhamisi.

Mnamo Alhamisi, Mahakama ya Sheria ya Shanzu ilimwachilia mwinjilisti huyo kwa bondi ya Sh3 milioni au dhamana ya pesa taslimu Sh1.5 milioni.

Alikamatwa kuhusiana na ibada ya Shakahola ambayo imesababisha vifo vya zaidi ya watu 100.

Ezekiel anatuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu, utakatishaji fedha haramu miongoni mwa madai mengine.