Inahuzunisha! "Nikienda nyumbani, natazama tu makaburi!" Rigathi afunguka upweke baada ya kakake kufariki

“Sasa nikirudi nyumbani huwa natazama tu makaburi, hakuna wa kuzungumza naye kwa sababu dada zangu walishaolewa," Rigathi alisema.

Muhtasari

•Rigathi alisema kuwa yeye na mkewe Dorcas Rigathi wamewekeza nguvu zao katika vita dhidi ya pombe kwani pia wao wamekuwa waathiriwa wa athari zake mbaya.

•Rigathi alisema alimuona kakake mkubwa mara ya mwisho akiwa hai wakati walipomtembelea baada ya kuapishwa kama naibu wa rais.

DP Gachagua
DP Gachagua
Image: HISANI

Naibu rais Rigathi Gachagua kwa mara nyingine amesisistiza kuhusu vita vyake dhidi ya pombe huku akibainisha kuwa hatua yake haina uhusiano wowote na siasa.

Akizungumza wakati wa mahojiano na Inooro TV siku ya Jumapili jioni, kiongozi huyo wa pili alisema kuwa yeye na mkewe Dorcas Rigathi wamewekeza nguvu zao katika vita dhidi ya dawa hiyo ya kulevya kwani pia wao wamekuwa waathiriwa wa athari zake mbaya.

Rigathi alitumia mahojiano hayo kusimulia kwa hisia kuhusu kifo cha marehemu kakake Jackson Reriani Gachagua ambaye alidai aliuawa na pombe.

“Ndugu yangu Reriani alikuwa mlevi. Nilijaribu kuzungumza naye na kumsihi ‘ndugu yangu tumeachwa wawili tu, nakuomba tafadhali usiniache peke yangu’ lakini hakusikia,” Rigathi alisimulia.

Bw Reriani alitangazwa kuwa amefariki katika Hospitali ya Jamii mjini Karatina mnamo Septemba 24, 2022 baada ya kuugua akiwa nyumbani kwake Mathira.

Jumapili, Rigathi alisimulia kwa hisia jinsi alivyomuona kakake mkubwa mara ya mwisho akiwa hai wakati walipokuwa wamemtembelea baada ya kuapishwa kama naibu wa rais.

"Yeye (kaka yake) alikunywa pombe, nilijaribu kumtibu katika hospitali ya hapa Karen, lakini alirudia ulevi," alisimulia.

Aliongeza, “Baada ya kuapishwa, mimi kama naibu wa rais, walikuja nyumbani kwangu hapa Nairobi na watu wengine. Walipokuwa wakienda nyumbani, kwa sababu nilifurahi sana, niliwapa kila mmoja kiasi kidogo cha pesa ili wale wakirudi nyumbani. Baadaye nilipata kumuona tena kwenye jeneza kwa sababu alienda kwenye pombe. Alienda kunywa pombe na akafa.”

Naibu rais alisema kifo cha aliyekuwa kakake mkubwa kilimuacha katika hali ya huzuni kwani sasa hana ndugu wa kuzungumza naye.

“Sasa nikirudi nyumbani huwa natazama tu makaburi, hakuna wa kuzungumza naye kwa sababu dada zangu walishaolewa. Dada zangu wote wameolewa. Katika nyumba nzima ya Gachagua, mimi ndiye pekee. Kuhusu Reriani, bado tungekuwa naye, kila nikienda nyumbani, nilikuwa napata mtu wa kuzungumza naye. Sasa niko peke yangu, ninaishi na polisi. Sina mtu kutoka kwa familia yetu, sina chochote. Ni polisi tu. Ninaporudi nyumbani, natazama tu makaburi,” alisema.

Rigathi pia alizungumza kuhusu kaka ya mkewe, Pastor Dorcas ambaye pia ni mlevi.

Alisema kwamba kuna watu wengine wengi ambao wameathiriwa na ulevi lakini wanateseka kimya kimya.

"Tunapopigana na pombe hii, sio siasa. Tunazungumza huku tukiwa na uchungu mwingi moyoni kwa sababu tumeona jinsi pombe ilivyotuumiza sisi, majirani na marafiki zetu,” alisema.