•Ombeta alidokeza kuwa kesi ya mchungaji huyo itaishia kwa yeye kuachiliwa ambapo baadaye atajitosa kwenye siasa na kufanikiwa.
•Alibainisha kuwa wakazi wa eneo la Shakahola watakuwa tayari kumpatia kura katika uchaguzi huo ujao
Wakili mashuhuri Cliff Ombeta ametoa maoni yake kuhusu sakata ambalo inayoendelea inayomhusisha mchungaji Paul MacKenzie.
MacKenzie anakabiliwa na shutuma nzito ambapo anadaiwa kuwadanganya mamia ya wafuasi wake kufunga hadi kufa ili ‘kukutana na Yesu’. MacKenzie bado yuko rumande baada ya korti kuwaruhusu polisi kuendelea kumshikilia ili kukamilisha ufukiaji wa miili yote iliyozikwa katika shamba lake huko Shakahola, kaunti ya Kilifi.
Akizungumza kwenye akaunti yake ya Twitter siku ya Jumanne, Ombeta hata hivyo alidokeza kuwa kesi ya mchungaji huyo itaishia kwa yeye kuachiliwa ambapo baadaye atajitosa kwenye siasa na kufanikiwa.
"Mchungaji Mackenzie atatoka na ataingia kwenye siasa mwaka wa 2027 na hakuna kitu mtafanya," aliandika.
Alibainisha kuwa wakazi wa eneo la Shakahola watakuwa tayari kumpatia kura katika uchaguzi huo ujao.
Wakili huyo alihoji jinsi serikali imejitayarisha kumshtaki MacKenzie na ushahidi gani walio nao dhidi yake.
"Miili iko hapa, roho ziko wapi? Tunathibitishaje kuwa haziko mbinguni? Jimbo linapata wapi mashahidi hao? Je, kuna njia ya kwenda mbinguni na kuthibitisha kwamba hawakufika huko?" Ombeta alihoji.
Aidha, mwanasheria huyo alibainisha kwamba mashtaka ya itikadi kali na ugaidi ambayo Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji ametayarisha dhidi ya mchungaji huyo mwenye utata yana lengo la kumzuia tu kupata dhamana ila sio kuthibitisha kwamba ana kesi ya kujibu.
Siku ya Jumanne, upande wa mashtaka ulipata maagizo mapya ya kuendelea kumzuilia mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie huku ikisubiriwa kukamilika kwa uchunguzi kuhusu dhehebu la itikadi kali la Shakahola.
Polisi mnamo Aprili 17 walipewa amri ya kumzuilia mhubiri huyo kwa siku 14 ambayo itakamilika Aprili 30. Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji alisema katika taarifa yake Jumanne kwamba uamuzi wa kumfungulia mashtaka Mackenzie utafanywa kulingana na matokeo baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
Mackenzie anadaiwa kuwashauri wafuasi wake wafunge ili wafe kwa njaa ikiwaahidi kuwa watakutana na Yesu.
Mkurugenzi wa Mashtaka alilaani kitendo hicho cha kinyama.
"Tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa familia na marafiki wa waathiriwa," Haji alisema.