Mgogoro wa Afya

Mudavadi:Serikali inafaa kushughulikia matakwa ya wahudumu wa afya

Muhtasari
  • Mudavadi amesema kuwa sio vyema kwa viongozi na hasa viongozi wa kisiasa kutamka matamshi ambayo huenda yakawachochea wahudumu wa afya kuwa na msimamo mkali 
  • Mudavadi alikuwa akizungumza katika wadi ya Wundanyi/Mbale katika eneo bunge la Wundanyi kaunti ya Taita Taveta alipokuwa akimpigia debe Julius Mwalicha Julia mgombeaji wa kiti cha Uakilishi Wadi (MCA) kwa tiketi ya chama cha ANC
Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi

Kinara wa chama ANC Musalia Mudavadi ameitaka Serikali kuu kupitia uongozi wake na hasa wizara ya afya kuangazia kwa haraka matakwa ya madaktari, wauguzi na wafanyikazi wengine katika sekta ya afya ili kuzuia hali ngumu ambayo huenda ikatokea kutokana na mgomo wa madaktari.

Mudavadi amesema kuwa sio vyema kwa viongozi na hasa viongozi wa kisiasa kutamka matamshi ambayo huenda yakawachochea wahudumu wa afya kuwa na msimamo mkali  hasa wakati huu ambapo wapo mstari wa mbele kulisaidia taifa kupambana na janga la ugonjwa wa Corona.

Kiongozi huyu wa chama cha ANC vile vile amewataka wakenya kuangazia suala zima la uongozi bora kwa kuwachagua viongozi ambao wana maono kwa wananchi hasa kuwahudumia wananchi bali sio viongozi ambao wakishachaguliwa wanayaweka maslahi yao mbele kabla ya maslahi ya wananchi.

Amesema kutompiga msasa kiongozi kabla ya kumchagua ndicho chanzo kikuu kinachosababisha kudorora kwa utoaji huduma kwa wananchi akitoa mfano wa jinsi baadhi ya magavana kwa sasa wanakumbwa na tishio la kuondolewa afisini kutokana na uongozi mbaya, ufisadi na uporaji wa mali ya umma pasi na kuwahudumia wananchi.

Mudavadi alikuwa akizungumza katika wadi ya Wundanyi/Mbale katika eneo bunge la Wundanyi kaunti ya Taita Taveta alipokuwa akimpigia debe Julius Mwalicha Julia mgombeaji wa kiti cha Uakilishi Wadi (MCA) kwa tiketi ya chama cha ANC. Uchaguzi huo mdogo utaandaliwa siku ya jumanne tarhe 15 mwezi disemba mwaka 2020 kwani kiti hicho kiliachwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa MCA Beatrice Mwabili kilichotokea mwezi machi mwaka huu.

Mudavadi alikuwa ameandamana na Mbunge wa Matuga Kassim Tandaza na Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama cha ANC Kelvin Lunani miongoni mwa viongozi wengine. Kuna jumla ya wagombeaji kumi na sita kwenye kinyang’anyiro hicho.