SRC kudhibiti marupurupu ya wafanyikazi wa serikali

Muhtasari

• Marupurupu hayafai kuzidi asilimia 60 ya mshahara.

• Pendekezo hili litaondolea serikali mzigo wa kima cha shilingi bilioni 100 kila mwaka.

• Aina 13 za marupurupu huchukua asilimia 80 ya malipo yote ya marupurupu.

GHARAMA: Mwenyekiti wa SRC Lyn Cherop Mengich wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu marupurupu ya nyumba ya wabunge mnamo Mei 15, 2019. Picha: ENOS TECHE
GHARAMA: Mwenyekiti wa SRC Lyn Cherop Mengich wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu marupurupu ya nyumba ya wabunge mnamo Mei 15, 2019. Picha: ENOS TECHE

Mshtuko unawasubiri wafanyikazi wa umma na maafisa wa serikali katika juhudi mpya za Tume ya Mishahara kudhibiti matumizi ya pesa za serikali.

Tume ya mishahara inataka marurupu yanayolipwa maafisa wa serikali na maafisa wengine wa umma kutozidi asilimia 60 ya mshahara wao.

Pendekezo hili huenda likamaliza shinikizo za kila mwaka za wafanyikazi wa umma na maafisa wakuu wa serikali kutaka nyongeza ya mshahara.

 

Pendekezo hili litaondolea serikali mzigo wa kima cha shilingi bilioni 100 kila mwaka wakati serikali inajaribu kusawazisha malipo ya wafanyikazi na kudhibiti gharama za matumizi ya pesa.

SRC inasema kwamba asilimia 48 ya bajeti ya kulipa mishahara ya sekta ya umma ni marupurupu yanayolipwa wafanyikazi wa serikali.

Aina 13 tu za marupurupu huchukua asilimia 80 ya malipo ya marupurupu yanayolipwa wafanyikazi wa umma.

SRC imechapisha miongozo ya rasimu ili kuhakikisha marupurupu yote yanayopewa wafanyikazi wa sekta ya umma yanalingana na michango yao halisi.

Kanuni hizi mpya zinasubiri mchango wa umma. SRC ina jukumu la kikatiba la kuweka mishahara na marupurupu kwa maafisa wa umma na serikali.