EACC yarejesha bilioni 6.3 zilizokuwa zimeibwa

Muhtasari

• Tume hiyo ilikuwa katika mchakato wa kukabidhi pesa hizo kwa serikali.

Mwenyekiti wa EACC Eliud Wabuhaka
Mwenyekiti wa EACC Eliud Wabuhaka

Tume ya Maadili na Kupambana na ufisadi mwaka huu imerejesha mali yenye thamani ya shilingi bilioni 6.1 bilioni na fedha taslimu shilingi milioni 209 katika vita dhidi ya ufisadi.

Akiongea wakati wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa, mwenyekiti wa EACC Eliud Wabukala siku ya Alhamisi alisema tume hiyo ilikuwa katika mchakato wa kukabidhi pesa hizo kwa serikali.

Wabukala alisema kuna haja ya kuimarisha urejeshwaji wa mali kwani itazuia ufisadi. Alisema tume hiyo itazingatia zaidi urejeshwaji wa mali kwani inadhihirisha kuwa ndio njia mwafaka ya kuzuia ufisadi.

"Tulipata nyumba mbili katika eneo la Woodley jijini Nairobi na hivi majuzi ardhi yenye thamani iliyokuwa imenyakuliwa kutoka idara ya hali ya hewa katika eneo la Viwandani yenye thamani ya Shilingi bilioni 5. Nimesikia kwamba serikali inakusudia kujenga nyumba za bei nafuu kwenye ardhi hiyo,"Wabukala alisema.

Vipande vingine vya ardhi na majengo pia vimepatikana katika eneo la Kisumu, Mtwapa, Kitale, Eldoret na eneo la Karen mjini Nairobi.

"Tutazidisha shughuli za aina hii. Kwa kweli hiki  kitakuwa kizuizi kwa wale wanaofaidika na kuchukua kutoka kwa umma. Lazima wapoteze kila kitu na hivyo kupoteza motisha,”akaongeza.

Wabukala alionyesha matumaini kuwa nchi inaweza kushinda vita dhidi ya ufisadi lakini "ikiwa tu Wakenya wataungana kupambana nayo."•