Ukatili! mwanamke akamatwa kwa kuingiza vijiti katika nyeti ya msichana mchanga

Muhtasari

• Aliripotiwa kushirikiana na bintiye kuingiza vijiti katika sehemu za siri za mtoto wa kike mwenye umri wa miezi 20 huko Machakos.

• Mtoto huyo mchanga alikuwa ameachwa chini ya uangalizi wa mshukiwa.

• Polisi wakisaidiwa na wenyeji walifanikiwa kumkamata mwanamke huyo na kumpeleka katika kituo cha polisi cha Matuu.

Polisi wamemkamata mwanamke aliyeripotiwa kushirikiana na bintiye kuingiza vijiti katika sehemu za siri za mtoto wa kike mwenye umri wa miezi 20 huko Machakos.

Shune Wawira mwenye umri wa miaka 23, kutoka Matuu, anadaiwa alimshawishi binti yake kuingiza vijiti ndani ya dada yake wa kambo kwa madai kwamba yeye hukojoa kitandani.

Mtuhumiwa ni mke mwenza wa mama wa mwathiriwa ambaye alikuwa amebaki na msichana huyo nyumbani kwao. Naibu Chifu wa eneo hilo Peter Muinde alisema mshukiwa anadaiwa kumtumia bintiye aliye na akili punguani kufanya unyama huo.

Msimamizi wa kijiji Jackline Mwilu alisema mtoto huyo mchanga alikuwa ameachwa chini ya uangalizi wa mshukiwa na binti yake wakati kisa hicho kilitokea Jumatano.

"Nilipata ripoti kwamba mwanamke alikuwa amefanya kitendo hiki cha kinyama kwa mtoto mchanga aliyekuwa ameachiwa kutunza na alikuwa anajaribu kutoroka", alisema.

OCPD wa Yatta Njoki Gachie alithibitisha kuwa msichana huyo aliingiza vijiti kwenye sehemu za siri za mtoto kwa urefu wa inchi 3 ambazo zilimwacha na majeraha mabaya.

"Msichana alikuwa anavuja damu sana tulipompata na tukamkimbiza hospitali ya Level 4 ya Matuu kwa huduma ya kwanza kabla ya kuhamishiwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta", Njoki alisema.

Polisi wakisaidiwa na wenyeji walifanikiwa kumkamata mwanamke huyo na kumpeleka katika kituo cha polisi cha Matuu kwa mahojiano huku uchunguzi ukiendelea.