Ruto akabiliana na Munya mazishini

Muhtasari

• Viongozi hao walikuwa katika mazishi ya mama wa mbunge wa Thika Patrick Wainaina.

• Itifaki ilivunjwa waziri Munya alizungumza baada ya Naibu rais kutoa hutuba yake.

• Munya alisoma hutuba na rais Uhuru Kenyatta, kwa kawaida hutuba hiyo ingesomwa na Ruto.

 

Naibu rais William Ruto (kushoto) na Waziri Peter Munya wakati wa ufunguzi wa kongamano ya uwekezaji Meru katika chuo kikuu cha KEMU. /DPPS
Naibu rais William Ruto (kushoto) na Waziri Peter Munya wakati wa ufunguzi wa kongamano ya uwekezaji Meru katika chuo kikuu cha KEMU. /DPPS

Naibu Rais William Ruto na Waziri wa Kilimo Peter Munya siku ya Jumanne walikabiliana hadharani mazishini katika kaunti ya Kiambu anakotoka Rais Uhuru Kenyatta.

Katika kile kilichoashiria mgawanyiko mkubwa kati ya Rais Kenyatta na naibu wake, Munya alimkosoa Ruto kuhusiana na matamshi yake ya awali kwamba baadhi ya viongozi wa eneo la Mlima Kenya walikuwa wakijaribu kumfanya Kenyatta kuwa Rais wa kanda.

“Rais Uhuru ni Rais wetu na ninataka kuwasihi ninyi kama viongozi na watu kutoka eneo hili, msimpunguze Rais kuwa Rais wa Mlima Kenya peke yake. Hapana.

"Ikiwa unasema Uhuru ni rais wa eneo hili pekee, ni nani atakuwa Rais wetu? Tulimpigia kura na tunampenda na tumeshirikiana naye miaka hii yote," Ruto alisema wakati akishangiliwa na baadhi ya waombolezaji.

Lakini akijibu madai ya Ruto, Munya ambaye alizungumza baada ya naibu rais alisema Uhuru ana haki ya kukutana na viongozi kutoka Mlima Kenya "kama atakavyofanya kwa maeneo mengine".

Alisema Rais amejitolea kuhakikisha kuwa kuna maendeleo katika maeneo yote ya nchi.

“Hatujawahi kusema Uhuru ni Rais wa eneo la Mlima Kenya peke yake. Yeye ndiye Rais wa Wakenya wote na tunamheshimu. Kama anavyotekeleza miradi ya maendeleo mahali pengine, anafanya pia kwa Mlima Kenya kwa sababu Mlima Kenya pia ni sehemu ya Kenya. Kwa hivyo hakuna shida kama vile Naibu Rais alisema, ”alisema.

Ruto na Munya pia walitofautiana vikali kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na utawala wa Jubilee katika ngome ya Uhuru.

DP ambaye alizungumza wakati wa mazishi ya mama wa mbunge wa Thika Patrick Wainaina eneo la Mang'u aliwauliza wanasiasa kutopunguza hadhi ya kitaifa ya Rais Uhuru Kenyatta kuwa ya kiongozi wa Mlima Kenya.

Alisema ni bahati mbaya kwamba viongozi wengine walikuwa wakimtaja Rais kuwa kiongozi wa kabila.

Ruto alisema hajawahi kujiona kama kiongozi wa Bonde la Ufa lakini mtumishi wa Wakenya wote.

Mbunge wa Gatundu Kaskazini Anne Wanjiku, ambaye alikuwa msimamizi wa zamu, alisoma miradi ambayo imesambazwa katika kaunti hiyo, pamoja na ile iliyokwama.

Wakati DP aliposimama, aliorodhesha pia barabara, maji na uunganishaji wa umeme ambayo imetekelezwa na kuahidi kwamba hatua zitachukuliwa kwa mkandarasi ambaye amekwamisha ujenzi wa barabara.

“Tutafanya kazi kwa bidii kutimiza ahadi tulizotoa  kama serikali ya Jubilee pamoja na barabara. Nakumbuka Kang’oo hadi Kamwangi kabla haijawekwa lami sasa imepewa lami, ”Ruto alisema.

Aliongeza, "Ni masikitiko kwamba mkandarasi aliyepewa barabara hajafanya barabara kama inavyotakiwa na ninataka kuhakikisha kuwa mkandarasi atapewa notisi na ikiwa hana uwezo, tuna kazi nyingi na wakandarasi wengi. Tutatafuta mkandarasi mwingine kutimiza ahadi tuliyoahidi, "Ruto alisema.

Hata hivyo, Munya alisema wakati wa mkutano wa hivi majuzi ambapo alikutana na wakulima wa kahawa na majani chai, aliambiwa juu ya barabara iliyokwama na mara moja akamjulisha Rais. Rais baadaye aliagiza waziri wa uchukuzi na Miundombinu James Macharia kuhakikisha mkandarasi anaanza tena kazi hiyo.

Katika mkutano huo ambao pia ulikumbwa na mkanganyiko wa kiitifaki wakati Ruto alimwalika waziri Munya kuzungumza hatua iliyofanya baadhi ya waombolezaji kutoka nje, Ruto aliwaambia watu wa Mlima Kenya kupuuza wale wanaochochea eneo hilo kwamba haheshimu Rais.

Ruto alisema anamuunga mkono Rais kikamilifu na amekuwa mshirika wake wa kuaminika kwa miaka mingi akiuliza wakaazi wa eneo hilo waachane na majaribio ya viongozi wengine.