BBI:Uhuru aongoza viongozi wengine kupongeza MCAs

Muhtasari

•  Uhuru aliungana na baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa katika Ikulu ya Nairobi ambapo walitoa taarifa  kupongeza mabunge ya Kaunti

Gideon Moi asoma taarifa ya viongozi wengine kupongeza mabunge ya kaunti wa kuidhinisha muswada wa marekebisho ya katiba
Gideon Moi asoma taarifa ya viongozi wengine kupongeza mabunge ya kaunti wa kuidhinisha muswada wa marekebisho ya katiba
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta siku ya Alhamisi aliongoza viongozi wengine wanaounga mkono mchakato wa BBI kupongeza  mabunge ya kaunti kwa kuidhinisha muswada wa marekebisho ya katiba 2020.

Rais Uhuru Kenyatta aliungana na baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa katika Ikulu ya Nairobi ambapo walitoa taarifa ya pamoja wakitoa shukrani zao kwa mabunge ya Kaunti ambayo yaliunga mkono Muswada wa BBI.

Viongozi hao wakiwemo Raila Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Gideon Moi (KANU), Charity Ngilu (Narc) na Moses Wetangula (Ford Kenya) walitoa wito kwa Wakenya wote kuunga mkono marekebisho hayo, wakisema kwamba yatatatua baadhi ya maswala ya muda mrefu yanayoathiri nchi.

"Leo, kwa niaba ya taifa lenye shukrani, tunatoa shukrani zetu kubwa kwa mabunge yetu yote ya Kaunti kwa msaada wao mkubwa kwa Mpango huu muhimu. Kitendo chao cha ujasiri kinaweka msingi ambao Kenya itaendeleza usawa wa vizazi, kutambua usawa wa kijinsia, kuhakikisha fursa sawa kwa wote, na kumpa kila Mkenya kipande kikubwa cha ustawi wetu wa pamoja, "ilisema taarifa ya pamoja iliyosomwa na Gideon Moi.

Kufikia siku ya Alhamisi muswada huo ulikuwa umeidhinishwa na kaunti 42 kati ya 47 na mabunge mawili tu  - Baringo na Nandi yaliopiga kura ya kupinga marekebisho hayo.

Vigogo hao wa kisiasa waliahidi kuanzisha zoezi la uhamasishaji wa umma kuhusu manufaa ya muswada huo na mchakati mzima wa BBI.

Viongozi wanaounha mkono mchakato wa BBI wamepanga kufanya mkutano wa pamoja wa mashauriano Machi 9, 2021, ikijumuisha wabunge na viongozi wa Kaunti.

“Kama vile Wawakilishi wetu wa Kaunti wameonyesha, sasa ni wakati wa Wakenya wote kuweka kando tofauti zao za vyama na kuja pamoja kujenga Kenya bora; kwa sisi wenyewe, watoto wetu, na kwa vizazi vya Wakenya ambao hawajazaliwa, ”ilihitimisha taarifa hiyo.