Sababu za ODM kuongeza makataa ya kutuma maombi ya urais

Muhtasari

• Ni gavana wa Mombasa Hassan Joho pekee aliyekuwa amewasilisha ombi lake.

• Hatua hiyo pia huenda ililenga kumpa gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya muda kuwasilisha ombi lake.

Catherine Mumma mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi ya ODM
Catherine Mumma mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi ya ODM
Image: HISANI

Chama cha ODM siku ya Alhamisi kiliongeza muda wa mwisho kwa wagombeaji wanaotaka kupeperusha bendera yake katika uchaguzi wa urais wa 2022.

Mwenyekiti wa Bodi ya kitaifa ya Uchaguzi Catherine Mumma alitangaza kuongeza muda wa zoezi hilo.

Kinara wa chama hicho Raila Odinga ambaye anatarajiwa sana kupeperusha bendera ya Chungwa hajawasilisha ombi lake na vile vile Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambaye pia alikuwa ameonyesha ari ya kutaka kuania nafasi hiyo.

Ni Gavana wa Mombasa Hassan Joho pekee ndiye aliyefanya amewasilisha ombi lake.

Bodi ya uchaguzi ya chama hicho haikutoa sababu za hatua yake ya mwisho, lakini duru zilieleza meza yetu ya habari kuwa hatua hiyo ilikuwa kumpa muda Oparanya ambaye anahusika katika uchaguzi mdogo wa Matungu.

Oparanya amekuwa akiongoza kampeni za mgombea wa Matungu David Were katika uchaguzi mdogo uliopangiwa kufanyika Machi 4.

"Oparanya amekuwa akiongoza kampeni zetu huko Matungu na kutokana na hali ya kampeni huko haikuwezekana kuja kuwasilisha fomu," afisa katika chama hicho alisema.

Mwenyekiti wa kitaifa wa ODM John Mbadi alisema uamuzi huo ni kuwapa wagombeaji wengine muda zaidi wa kuwasilisha maombi yao.

"Wagombea wengine waliovutiwa waliomba muda zaidi," Mbadi alisema kwa simu.

Siku ya Alhamisi, mwenyekiti wa uchaguzi Catherine Mumma alitangaza kuwa wanaotaka nafasi hiyo wana hadi Machi 31 kuwasilisha maombi yao.

"Wagombea wote wanaovutiwa wanahitajika kuwasilisha maombi yao kwa njia iliyoamriwa”. Mumma alisema.