Mfanyikazi wa tume ya ardhi Jennifer Wambua alinyongwa

Muhtasari

• Upasuaji wa mwili wa Jennifer Wambua umebaini kwamba aliuawa kwa kunyongwa.

• Mwili pia ulikuwa na michubuko mingine usoni na miguuni.

Maafisa wa DCI baada ya kuuweka mwili wa marehemu Jennifer Wambua kwenye gari katika City Mortuary, Nairobi, Machi 15, 2021.
Maafisa wa DCI baada ya kuuweka mwili wa marehemu Jennifer Wambua kwenye gari katika City Mortuary, Nairobi, Machi 15, 2021.
Image: ANDREW KASUKU

Upasuaji wa mwili wa mfanyikazi wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC)aliyepatikana akiwa amefariki Jennifer Itumbi Wambua umebaini kwamba aliuawa kwa kunyongwa.

Uchunguzi wa maiti ulifanywa siku  ya Alhamisi katika hifadhi ya maiti ya Montezuma Monalisa mjini Nirobi.

Matokeo ya uchunguzi wa maiti uliofanywa na mwanapatholojia wa serikali Johannsen Oduor yalitangazwa na wakili Daniel Maanzo (Mbunge Makueni).

Alisema mwanapatholojia alieleza familia kuwa Jennifer alinyongwa kwa kutumia mikono pekee.

"Koo lake lilikuwa limefinyika ishara kwamba alikuwa amenyongwa kwa kutumia mikono," alisema.

Mwili pia ulikuwa na michubuko mingine usoni na miguuni na Oduor alisema uchunguzi zaidi utafanywa ili kubaini ikiwa alibakwa.

Matokeo haya yalijiri wakati polisi walisema wanachunguza uwezekano wa mwanahabari huyo ambaye alikuwa naibu mkurugenzi wa mawasiliano katika tume ya NLC kushawishiwa na mtu aliyemjua na kutekwa nyara kabla ya kuuawa.

Wapelelezi wanaoshughulikia suala hilo wanasema hiyo ni moja ya nadharia wanayoifuata.

Wanapanga kuzungumza na wenzake kazini, marafiki, familia na mtu mwingine yeyote ambaye anaweza kusaidia kufunua kitendawili cha mauaji yake.

"Kuna uwezekano kwamba aliambiwa mapema na akaitisha mkutano nje ya ofisi. Huenda aliambiwa asibebe simu yake ya mkononi kwenda kwenye mkutano kwani ingemfichua.”

"Inawezekana aliangukia kwenye mtego huu na akaacha begi lake ndani ya gari na kutembea kuelekea kwenye mkutano ambao uligeuka kuwa njama," afisa mmoja alisema.