Mudavadi amuomboleza marehemu rais Magufuli

Muhtasari

• Kinara wa ANC Musalia Mudavadi alisema alipokea ujumbe wa kifo cha Rais wa Muungano wa Jamhuri ya Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa huzuni mwingi.

Marehemu rais John Pombe Magufuli
Marehemu rais John Pombe Magufuli

Viongozi mbali mbali kutoka pembe zote za dunia wameendelea kutuma risala zao za rambi rambi kwa familia na taifa la Tanzania kufuatia kifo cha rais John Pombe Magufuli.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi alisema alipokea ujumbe wa kifo cha Rais wa Muungano wa Jamhuri ya Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa huzuni mwingi.

Alisema Rais Magufuli alikuwa kiongozi shupavu, aliyeheshimika na misimamo ya maamuzi yake haikuwa ya kutiliwa mzaha.

“Alikuwa kiongozi aliyezingatia demokrasia, maadili na jukumu kuu likiwa kuwahudumia wananchi kupitia utumishi kwa umma. Pombe alikuwa kiongozi aliyezingatia pakubwa ukuaji wa uchumi na alitilia mkazo ukuaji wa muungano wa umoja wa ukanda wa Afrika Mashariki,” Mudavadi alisema.

Mudavadi alikariri kuwa Magufuli alienziwa pakubwa kutokana na ucheshi wake, vigezo vyake vikiashiria pakubwa ukwasi aliounata kwenye historia na tamaduni za kiafrika.

“Kama taifa la Kenya tutamkumbuka kama kiongozi aliyeyajali maslahi ya kila mwananchi, mtetezi wa haki bila ya kubagua wala kuegemea upande wowote. Pole zangu kwa mke wake Mama Janeth Magufuli, familia, ndugu, jamaa na marafiki na kwa ujumla Jamhuri ya Tanzania kwa kumpoteza kiongozi aliyegusa nafsi kwa njia moja au nyingine”, Mudavadi aliongeza.