Tanzania: Makamu wa rais Samia Suluhu kuapishwa leo kama rais

Muhtasari

• Samia Suluhu Hassan mwenye umri wa miaka 61,atakuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huu nchini Tanzania na wa pili Afrika Mashariki.

Makamu wa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuapishwa wakati wowote kutoka sasa kuchukuwa wadhifa wa rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania katika Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Samia Suluhu Hassan mwenye umri wa miaka 61,atakuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huu nchini Tanzania na wa pili Afrika Mashariki.

Samia atashikilia wadhifa huo kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa urais mpaka 2025, kwa mujibu wa katiba ya Tanzania.

Slyvie Kiningi ndiye alikuwa rais wa pekee mwanamke aliyehudumu kama rais kanda ya Afrika Mashariki nchini Burundi.

Wadhifa wa rais wa Tanzania ulisalia wazi baada ya kifo cha aliyekuwa rais John Pombe Magufuli ambaye kulingana na taarifa ya serikali alikuwa na matatizo ya moyo Jumatano, Machi 17, 2021.

Kwa mujibu wa kifungu cha 37 (5) cha Katiba ya nchi hiyo, nafasi ya urais inapokuwa wazi kwa sababu yoyote ikiwemo kifo, viongozi watatu wameorodheshwa na ni Makamu wa Rais, na endapo hatakuwepo atachukua Spika wa Bunge na kama hayupo atachukua Jaji Mkuu.

Suluhi alizaliwa Januari 27, 1960 katika eneo la Zanzibar na kumaliza elimu yake ya sekondari mwaka 1977.

Huku akifanya kozi mbali mbali, Suluhu aliteuliwa kuwa karani katika wizara ya mipango na maendeleo.

Alipata Diploma kutoka chuo Kikuu cha Mzumbe na kisha kupata kazi katika shirika la chakula duniani (WFO).