Wiper yaonyesha UDA kivumbi Machakos

Muhtasari

• Kavindu alizoa kura 104,082 na kumshinda kwa mbali mpinzani wake wa karibu Urbanus Ngengele wa chama cha UDA aliyepata kura 19,705.

Agnes Kavindu akipiga kura katika uchaguzi wa seneta wa Machakos
Agnes Kavindu akipiga kura katika uchaguzi wa seneta wa Machakos

Mgombeaji wa chama cha Wiper Agnes Kavindu ameshinda uchaguzi mdogo wa kutafuta seneta wa Machakos.

Kavindu alizoa kura 104,082 na kumshinda kwa mbali mpinzani wake wa karibu Urbanus Ngengele wa chama cha UDA aliyepata kura 19,705.

Uchaguzi huo uliandaliwa siku ya Alhamisi na ulikuwa wa amani ikilinganishwa na chaguzi zingine ndogo zilizofanyika hivi majuzi.

Kiti cha seneta wa Machakos kilisalia wazi baada ya kifo cha ghafla cha aliyekuwa seneta Boniface Kabaka, Disemba mwaka uliyopita.

Kavindu ambaye kampeni zake ziliongozwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka aliungwa mkono pia na vyama vya Kanu, ANC, FORD Kenya, ODM na hata mgombeaji wa chama cha Maendeleo Chap Chap Mutua Katuku alijiondoa kutoka uchaguzi huo na kumuunga mkono Kavindu.