Mazishi ya marehemu mbunge Paul Koinange kufanyika Jumamosi

Muhtasari

• Familia hiyo katika taarifa yake ilisema kwamba itafuata masharti yote ya serikali kuhusu udhibiti wa maambukizi ya virusi vya corona.

• Misa ya wafu ya marehemu itafanyika katika kanisa la St. John Kiambaa kuanzia mwendo wa saa tano mchana kwa muda usiyozidi saa moja.

Marehemu mbunge wa Kiambaa Paul Koinange.
Marehemu mbunge wa Kiambaa Paul Koinange.
Image: MAKTABA

Familia ya marehemu mbunge wa Kiambaa Paul Koinange imetangaza kwamba atazikwa siku ya Jumamosi Aprili 3.

Familia hiyo katika taarifa yake ilisema kwamba itafuata masharti yote ya serikali kuhusu udhibiti wa maambukizi ya virusi vya corona.

Misa ya wafu ya marehemu itafanyika katika kanisa la St. John Kiambaa kuanzia mwendo wa saa tano mchana kwa muda usiyozidi saa moja.

Familia vile vile ilisema kwamba baada ya maombi, mazishi ya mbunge huyo yatafanyika nyumbani kwake Kiambaa katika hafla itakayo hudhuriwa tu jamaa zake.

Watu 50 pekee wataruhusiwa kuhudhuria mazishi hayo kuzingatia kanuni za wizara ya afya.

“Tungependa sana kumfanyia marehemu mheshimiwa Paul Koinange mazishi yanayostahiki hadhi yake, lakini kwa sababu ya masharti ya serikali lazima tuyafuate,” taarifa hiyo ilieleza. 

Mrehemu Koinange alifariki mapema siku ya Jumatano akipokea matibabu kutokana na athari za Covid-19.

Kufikia kifo chake alikuwa mwenyekiti wa kamati ya bunge ya utawala na usalama wa kitaifa.