Nyambizi ya Indonesia yapatikana imekatika vipande vitatu chini ya bahari

Muhtasari

• Wanajeshi wote 53 waliokuwa ndani ya nyambizi hiyo wamethibitishwa kufariki.

• Nyambizi hiyo kwa jina KRI Nanggala ilitoweka baada ya kuomba rukhusu kupiga mbizi wakati wa mazoezi ya torpedo. Sababu za kuzama kwake haijulikani.

PIcha za chini ya maji zinaonesha nyambizi uliopasuka vipande vipande
PIcha za chini ya maji zinaonesha nyambizi uliopasuka vipande vipande
Image: EPA

Nyambizi ya jeshi la wanamaji nchini Indonesia iliyotoweka katika pwani ya mji wa Bali siku ya Jumatano imepatikana ikiwa imekatika vipande vitatu chini ya bahari , maafisa wamesema.

Wanajeshi wote 53 waliokuwa ndani ya nyambizi hiyo wamethibitishwa kufariki.

Maafisa wa wanamaji wanasema kwamba walipokea ishara katika eneo ilipokuwepo manuwari hiyo zaidi ya kina cha mita 800 mapema Jumapili.

Gari la uokoaji wa chini ya maji lililokodishwa kutoka Singapore lilitumwa chini ya maji kuthibitisha picha ya mabaki ya manowari hiyo.

Nyambizi hiyo kwa jina KRI Nanggala ilitoweka baada ya kuomba rukhusu kupiga mbizi wakati wa mazoezi ya torpedo. Sababu za kuzama kwake haijulikani.

Sare za kujinusuru zinazoaminika kutoka katika nyambizi hiyo ya wanamaji wa KRI Nanggala
Sare za kujinusuru zinazoaminika kutoka katika nyambizi hiyo ya wanamaji wa KRI Nanggala
Image: REUTERS

Taarifa ya siku ya Jumapili ilijiri siku moja baada ya jeshi la India kuthibitisha kwamba mabaki ya nyambizi hiyo ikiwemo mikeka ya kusali ilipatikana katika eneo ambalo ilitoweka.

Mkuu wa jeshi la wanamaji Yudo Margono alisema kwamba vifaa zaidi kutoka kwa nyambizi hiyo vilipatikana ikiwemo sare za usalama za nahodha na wafanyakazi.

''Nyambizi ya KRI Nanggala imegawanywa mara tatu, ganda la meli, nyuma ya meli, na sehemu kuu zote zimetengwa, huku sehemu kuu ikipatikana imepasuka'', aliambia waandishiwa habari siku ya Jumapili.

KRI Nanggala 402 graphic

Mkuu wa jeshi la Indonesia Hadi Tjahjanto , alithibitisha kwamba hakuna uwezekano wa kuwapata wanajeshi hao wakiwa hai.

''Kwa huzuni mkubwa ninaweza kusema kwamba wanajeshi wote 53 waliokuwa wakiabiri chombo hiki wamefariki'', aliambia wanahabari.

Wataalamu walikuwa wamesema mapema kwamba kina ambacho nyambizi hiyo ilipatikana kilikuwa juu ya uwezo wa manuwari hiyo kunusurika na kwamba ilikuwa imebeba oksijeni ya kukimu siku tatu pekee.

Familia za wanajeshi waliotoweka katika ofisi za Koarmada 11 katika eneo la Surabaya , mashariki mwa mkoa wa Java Indonesia Aprili 25 2021
Familia za wanajeshi waliotoweka katika ofisi za Koarmada 11 katika eneo la Surabaya , mashariki mwa mkoa wa Java Indonesia Aprili 25 2021
Image: REUTERS

Rais Joko Widodo aliwataja wanajeshi hao kama wazalendo wakuu wa Indonesia , akiongezea: Raia wote wa Indonesia wanatuma risala za rambirambi kuhusu tukio hili hususan kwa familia za wanajeshi waliofariki."

Kutoweka kwa KRI Nanggala kulivutia operesheni ya usakaji wake kimataifa huku Marekani, Australia, Singapore, Malaysia na India zikitoa usaidizi.

Nyambizi hiyo iliotengenezwa nchini Ujerumani ilikuwa na zaidi ya miaka 40 lakini ilifanyiwa ukarabati 2012.

Ramani ya Indonesia na eneo ambalo nyambizi hiyo ilizama
Ramani ya Indonesia na eneo ambalo nyambizi hiyo ilizama